Nguvu ya kuzaliwa - kwasababu alizaliwa


Jesus Up!

Asingezaliwa basi asingekufa, kanuni ingekataa. Asingezaliwa asingeishi duniani maana kanuni haikubali kuishi bila kuzaliwa. Asingezaliwa asingevaa nguo maana vya mwili ni kwa mwili tu. Asingezaliwa asingeitwa jina maana isingefaa kitu kuwa na jina bila kuonekana duniani. Asingezaliwa asingekuwa na wazazi. Asingezaliwa asingekuwepo duniani na asingefanya lolote. Asingezaliwa asingelia. Asingezaliwa asingeona kiu au njaa au maumivu au kuchoka. Asingezaliwa nani angempinga ili lile alilokuja kulifanya litimie? Asingezaliwa asingekimbilia Afrika kujificha na kujiokoa na adui yake. Asingezaliwa nguo yake isingegombaniwa maana asingekuwa nayo. Asingezaliwa historia yake isingeandikwa na nani angeisoma kama isingekuwepo popote? Asingezaliwa nani angemjua katika mwili? Nani angemsaidia kazi alokuja kufanya? Yote haya yanawezekana kwakuwa nguvu ya kuzaliwa ni kwasababu alizaliwa.

Ndio, nitumie sehemu hii ya kwanza kwenda sambamba na kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambako sisemi alizaliwa tarehe 25.12, hapana ila kama kumbukumbu ya kuzaliwa kwake. Kikubwa ni kwamba kwakuwa alizaliwa, akaishi na kufanya kazi na kupata mateso mpaka mauti ya msalaba lakini akafufuka mwisho wa siku kwa hiyo kumbukumbu hii ina maana kwani inamuhusu mtu aliye hai hata sasa. Unaweza ukawa umeadhimisha siku hii kwa njia mbali mbali lakini ukakosea pointi za muhimu maana Yesu Kristo Bwana alishazaliwa zamani za kale. Kila jambo alilolifanya na ambalo tunamsifia na kumkubali nalo leo hii ni kwasababu alizaliwa. Hakika, nguvu ya kuzaliwa kwa Bwana na Mowokozi wetu. Ni kweli alizaliwa na bikira. Alizaliwa kwa uwezo wa Mungu mwenyewe. Unaweza kupinga na kugalagala lakini utazidi kuumia tu na kujikwaza maana kuhusu Bwana Yesu ni fumbo la imani na kwazo la mataifa. Kwa uwezo wa Mungu Bwana Yesu alizaliwa. Alizaliwa toka kwenye kabila ambalo halikutegemewa kumleta masihi. Alizaliwa katika mazingira magumu ambayo sio ya kifahari na wala hayatii moyo kwa lolote. Alizaliwa kwa uwezo wa Mungu kwa namna ambayo huwezi kuiga lakini kwa namna ambayo haiwezi kueleweka kwa mtu aisiyetayari kuelewa. Alizaliwa kwa kusudi. Alizaliwa kwa sababa. Alizaliwa kwa malengo. Alizaliwa kwa ajili ya watu. Alizaliwa awafie watu. Alizaliwa ili afe, ndio yaani auwawe maana katika kifo ndo ulikuwa ushindi wake. Alizaliwa ili afufuke. Alizaliwa ili atukomboe.

Si unajua hata wanaompinga ni kwasababu alizaliwa? Kumpinga kwao hakuondoi ile KWELI kuhusu yeye. Kumpinga hakujamfanya abadilike kwa lolote. Bali kwasababu alizaliwa basi ilibidi apite katika yote aliyokwisha kuandaliwa. Sijui ingekuwa wewe au mimi tungefanyaje. Kwenye lile somo jingine nimeandika KUNA MAMBO UNGEYAJUA KABLA HUJAZALIWA USINGEKUBALI KUZALIWA, lakini yeye alijua yote yatakayompata nab ado akakubali kuja kuzaliwa kama mwanadamu wa kawaida na kupitia aibu na mateso yote. Alijua atakosa mahali pa kuzaliwa lakini bado akaja kuzaliwa. Alijiua atateswa kwa makosa yasiyo yake lakini bado akawa tayari kuja kuzaliwa. Kwake, kuja kuzaliwa ilimaanisha kuwa yuko tayari pia kufia sababu ya kuzaliwa kwake. Aliyajua yote lakini bado akaja kuzaliwa duniani.

Kifurushi cha kusudi la kuzaliwa kwake, yaani nguvu ya kuzaliwa kwake ilibeba mpaka jina lake. Asingezaliwa asingepewa jina. Kwasababu ya kazi yake jina mmoja halimtoshi. Basi kutokana na uwezo wake wa kushauri na kutatuta matatizo sugu hata kabla hajazaliwa miaka kama 700 hivi kabla ya kuzaliwa kwake aliitwa Mshauri wa Ajabu. Huyo huyo ni Mfalme wa Amani. Unaweza ukamuita pia Baba wa milele. Ana nguvu za kutosha na kwahiyo aliitwa pia Mungu mwenye nguvu ambaye uweza wa kifalme uko mabegani mwake. Hakuna mtu kwenye historia ambae utabiri wake, yaani angezaliwaje, angezaliwa na nani na kwanini angezaliwa, yote hayo yakawa yamesemwa miaka zaidi ya 700 kabla ya kuzaliwa kwake. Miaka zaidi ya 700 kabla ya kuzaliwa kwake ilijulikana maisha atakayoishi, kwamba hatashauriwa kwa hekima za kibinadamu, pia ilijulikana angepata mateso yote ambayo hakuna mwanadamu ameshawahi kuyapata hapa duniani. Kwasababu alizaliwa, kuzaliwa kwakekulimaanisha uhuru wa watu wengi. Huyu ni Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wa wanadamu toka katika vifungo vyao vyote. Huyu ndo ile kweli. Ile kweli ambayo ina nguvu za kumuweka mtu huru.

Alijua atatemewa mate lakini alikuwa tayari na akakubali kuzaliwa. Mangapi ambayo huwa unayaona magumu katika historia ya Bwana Yesu lakini bado alikubali kuzaliwa akimaanisha yuko tayari kufa na kama ungekuwa wewe ungekubali? Alijua rafiki zake wa karibu watamsaliti na kumgeuka lakini bado alikuwa tayari kufa kwa ajili yao, yaani ingekuwa mimi sijui kama ningekubali. Kumfia mtu ameniboa na kunidharau na kunikimbia wakati wa shida, ingekuwa haieleweki. Alijua ndugu zake watamwona ana kichaa lakini bado alikubali kuzaliwa na hao ndugu pamoja. Alijua kuwa atapigiliwa misumari mikononi na miguuni lakini bado alikubali na tena kuja kuwafia hao hao wanaomtesa. Alijua kuwa atapigwa mijeledi na atajeruhiwa kwa makosa yasiyo yake lakini akakubali kuzaliwa ili ayafie makosa ya wengi. Alijua kuwa lazima apate kipigo toka kwa watu ambao anawafia pia lakini alikuwa tayari kuja kuzaliwa na kufa kwa ajili yao. Bwana Yesu wewe ni wa ajabu sana. Wewe sio wa kawaida. Nani anafanana na wewe? Nisingeweza kwakweli.


Ni kwasababu alizaliwa ndo maana leo mimi pamoja na wale waaminio wako huru na mateso na magonjwa ya kila aina. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana wapo wanaodharau kuwa hakuna wokovu duniani. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana wapo wanaojifanya wao ni zaidi yake ingawa wote walikufa na wanakufa na hawarudi. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana ilibidi azaliwe. Wapo waliomuiga lakini kwakuwa yeye si wao basi wameishia kuabika. Aliyoyafanya yameandika historia ambayo hakuna mwanadamu anaweza kuifuta au kuivunja. Na hii yote ni kwasababu alizaliwa.

Hakuzaliwa kwa bahati mbaya kama wengi wanavyoiweka ili wajisikie vizuri.Hakuzaliwa kama ajali. Hakuzaliwa kama mkosi. Hakuzaliwa kwa ajili ya watu fulani maalum. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana tunajua kuwa kuzaliwa kwake kulitabiriwa miaka mingi sana kabla ya kuja kwake. Hakuna mwanadamu mwenye historia kama yake. Kuzaliwa kwake kulikuwa ni mpango kamili wa ukombozi. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana vipofu wanaona na viwete wanatembea, ni kwasababu alizaliwa ndo maana wafu wanafufuliwa. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana nimeokoka. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana alikufa. Ni kwasabu alizaliwa ndo maana alifufuka. Ni kwasababu alizaliwa ndo maana atarudi tena kuja kukamilisha mpango wa kumaliza kazi. Nielewe tu kuwa ni kwasababu alizaliwa. Kumkataa hakupunguzi lolote ndani yake. Kumpinga hakumfanyi awe wewe. Kumdharau hakukufanyi uwe bora kuliko wewe. Unapokumbuka kuzaliwa kwake fahamu kuwa ni kwasababu alizaliwa na bila hiyo hali zetu zingekuwa za ajabu sana.

Nguvu ya kuzaliwa ni kubwa kuliko kuzaliwa kwenyewe, yaani kuzaliwa kulimaanisha mengi zaidi ya kuzaliwa tu. Wengi husau kuwa njia pekee ya kutokufa ni kutokuzaliwa lakini kwakuwa umezaliwa basi kufa hakukwepeki ni lazima. Ndio njia ya kuthibitisha kuwa ulizaliwa na umemaliza kazi. Unaweza ukajiuliza mengi pia kuhusu wewe na maisha yako yote. Au niseme ukijiuliza kwa namna hii ya nguvu ya kuzaliwa, unaona na kupata nini kuhusu maisha yako? Je, kuzaliwa kwako kuna maana yoyote? Je, unajisikia vizuri kwamba ulizaliwa? Yako mengi ya kujiuliza.

Ni kwasababu nilizaliwa ndo maana naishi mpaka leo. Ni kwasababu nilizaliwa ndo maana naandika nguvu ya kuzaliwa, mfululizo mrefu unaoyaleta maisha yako katika uelewa wa karibu sana kwako. Ni kwasababu nilizaliwa ndo maana nitakufa siku moja kwenda kwenye utukufu mkuu zaidi. Ni kwaababu nilizaliwa ndo maana nilianzisha maono ya YKM. Ni kwasababu nilizaliwa ndo maana nitafanya Exposing Founders. Ni kwasababu nilizaliwa ndo maana ninaweza kusafiri. Kumbe maisha yangu yana kusudi kubwa zaidi ya kuzaliwa kwenyewe, yaani ilibidi nizaliwe ili ndo iwe na maana. Kuna mambo huwezi kuyafanya kama hujazaliwa. Kama hujazaliwa huwezi kuishi duniani katika mwili. Kama hujazaliwa huwezi kufa. Kama hujazaliwa huwezi kuishi.

Jikague. Jipime. Jitafute. Jiulize.

By Raphael Joachim Lyela

YKM Founder

Box 3613.

Dodoma.

www.ykmjesusup.org

Maoni