HERI WENYE NJAA, KIU, HAMU NA SHAUKU ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli maana hao ndio waabudu halisi ambao tamaa yao ni MUNGU. Ulimwengu tunaoishi na mambo tunayokutana nayo, mengi sana hutukatisha tamaa na kuondoa shauku na kiu na hamu ya KUMWABUDU MUNGU wa kweli katika roho na kweli. Tuna dhiki za kututosha, changamoto na starehe za maisha kwa namna ambayo usipokuwa makini utajikuta umepoa kwa ndani ingawa huku nje unaonekana uko hai. Usipokuwa makini unaweza ukajikuta UNAWABURUDISHA watu sana kwa uimbaji wako na huku wewe mwenyewe HUBADILIKI hata nukta moja na kwahiyo hata wale wanaoburudika wanabaki kuburudika tu. Hii ni siri nzito. Ni kweli unakuwa unaimba maana una sauti nzuri na ya kuvutia, ni kweli unapiga vyombo vyote, ni kweli kabisa unaweza ukamiliki stage, ila usipokuwa makini utaendelea kumiliki stage na ukashindwa kuumiliki moyo. Moyo wa mwanadamu ni mdanganyifu sana, maana hata hapa ninapoandika najiona kabisa moyoni mwangu kuwa mimi ni muhitaji sana, nimepungukiwa sana lakini bado naiona vita ambayo mtu wa nje hawezi kuiona maana iko ndani yangu. Kiu ya kumtafuta Mungu ipo, ila kumtafuta inakuwa ishu. Shauku ya kuomba ipo, ila siombi. Nina njaa na NENO lake ila silisomi. Huu ni umasikini wa roho ambao unadhihirisha uhitaji. Ni wazi kuwa Mwabudu Halisi anajitambua na anajua kuwa mazingira ya KUMTAKA Mungu hutengenezwa ila kama shauku imepotea basi kazi ipo kweli kweli. Wewe fikiria, unakuwa na shauku na hamu ya kuwahi kuchaji simu ili uendelee kuchat na unasubiria simu ikionyesha tu alama ya chaji unaiwasha ili uendelee kuchat badala ya kutumia basi hata ule muda simu ina chaji ili UICHAJI ROHO YAKO. Yaani, ona jinsi inavyokuwa rahisi kujenga hata shauku ya kuimba maana unajua kuna watu watakusikiliza na mwisho watakushangilia na kulike video yako youtube lakini wewe mwenyewe huna hata muda wa KUMSIKILIZA JEHOVA MUNGU hata kwa nidhamu ya kuzima simu. Unajiuliza, hivi mimi ni mtu wa namna gani ambae simu unakaa nayo masaa 24 ikiwa on na unachat na watu siku nzima mpaka ukiwa chooni na ukitaka kuomba pia unaiweka tu silent huku moyo wako ukiangalia mara kwa mara kama kuna msh imeignia au la. Nisikilize, SHAUKU INAJENGWA KWA MAZOEZI,yaani kama huna shauku ya kuomba anza kuomba ukiwa kwenye hali hiyo hiyo.Ukiona huwezi basi soma biblia mahali ambapo panaweza kukuinua ili uone haja ya kuomba. Ukiona una shauku ya kuimba kuliko shauku ya KUMLINGANA BWANA ujue hakika wewe ni MBURUDISHAJI,yaani wewe ni shabiki wa umaarufu, yaani wewe ni mfuasi wa idara ya KAPU LA UJINGA. Ni sawa na kuwa na shauku ya kucheza step na kukatika na hata kuiga step za matango ya porini na kuzileta kanisani na kuziita DISKO LA YESU-ACHA UJINGA, YESU HANA DISCKO. Nasema haya yakiniuma maana ujinga una wafuasi wengi kama utumwa na wala sio lazima iwe wewe kwani WAABUDU HALISI ni wachache kwa kiwango ambacho Mungu anawatafuta. Ninachotaka kusema ni hiki, kumwabudu Mungu katika roho na kweli kunahitaji kujijenga na kujijengea maisha ambayo UTAJITIA MOYO MWENYEWE hata kama mazingira hayakubali kwani kiu na shauku ni msingi wa kujihimiza kufanya. Na kwakuwa dunia imeweka mazingira ya kutuondoa kwenye kumuabudu EL SHADAI basi ni wazi kuwa ipo kazi ya kufanya. Hebu elewa Warumi 12:2, USIIFUATISHE NAMNA YA DUNIA HII,usijifanye umeelewa ukapitiliza na usijifanya hujaelewa ukapuuzia ili uendelee kufanya ulokuwa unafanya jana. Dunia hii ina NAMNA yake, yaani mifumo yake na maisha. Mwabudu Halisi anajua kuwa dunia ina mavazi yake, ina stepu zake, ina nyimbo zake, ina muziki wake na ina kila kitu cha kwake na sisi hatutakiwi KUIGA. Kazi ni kwako. Leo unaweza ukajipima tena. SHAUKU yako ya kumtafuta Mungu imemezwa na nini? Ile kiu ulokuwa nayo ya kutaka kutembea na Mungu mwaka huu wote imefukiwa na nini? Ulisema una njaa na Neno la Mungu, umeshiba nini kingine? Ulisema una hamu ya uwepo wa Mungu, mbona unafurahia uwepo wa sifa za wajinga na umeridhika? KUBADILIKA NI MAAMUZI YAKO ila usisahau UJINGA NA UTUMWA vina wateja wengi sana. Heart2Heart Worship Moments by Raphael JL:
Maoni
Chapisha Maoni