UBAYA WA WATU UKO NDANI YA MTU
Ubaya ulio ndani ya mtu una nguvu na uwezo wa kuambukiza
namna hiyohiyo ya kuwaona hata watu wengine kuwa ni wabaya. Ni sawa na kusema,
mganga wa kienyeji hachelewi kuwaona wengine wote pia kuwa ni waganga ila yeye
amewazidi uwezo au nguvu. Ni rahisi sana kwa mwizi kuwaona na wengine ni kama
yeye maana uzuri au ubaya unaanzia ndani ya mtu husika. Mwanaume asiye
mwaminifu kwa mkewe ni rahisi sana kuona kuwa hata mkewe pia hajatulia kama
yeye. Hii ni kanuni,ubaya wa watu uko ndani ya mtu kwanza kabla haujatoka nje. Cha
ajabu ni kwamba namna hii ya mfumo wa kufikiri mara nyingi hutokea kwa upande
wa mambo mabaya na sio mazuri. Kwa mfano ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida
kuwaona wengine ni waaminifu eti tu kwa sababu yeye ni mwaminifu. Ni wazi pia
kuwa HUWEZI KUTOA USICHOKUWA NACHO, ila inategemea sana ulichonacho ni nini na
kina ubora wa namna gani. Basi leo tuitazame kanuni hii kwa undani kama Neno la
Mungu linavyotufunulia siri hii.
Mathayo 6:1-18.
Kuna mambo matatu yameandikwa ndani ya mistari hii, ambayo
yamejengwa kwenye kanuni moja kubwa sana. kanuni hii imenichangamotisha sana na
kunifanya niwaze na kujikagua na kujipima na kujiona kama nikipimwa nitakuwa
kwenye mizani ipi. Kanuni yenyewe inasema hivi, angalieni msifanye wema wenu
machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati
thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Matahyo 6:1
Ukisoma kwa kuendelea hapo chini mapaka msitari wa 18, utaona
mambo matatu yaliyotajwa moja kwa moja yayakiunganishwa na kanuni yenyewe
ambayo imetaja WEMA kwa ujumla wake. Na hapo kufanya wema inaweza ikawa
inaeleweka kwa namna nyingi sana maana ni jumla ya kila aina ya mambo unayotaka
au kutamani kuyafanya kwa watu hata kama ni kuwapa msaada, au kuwashauri au
kuwatia moyo au vyovyote vile unaweza kuiweka hapo. kikubwa ni kujua kuwa yako
mambo ambayo kanuni imeyabeba na ambayo ndiyo hasa msingi wa somo hili la leo.
Niseme machache kwanza kabla sijafika mbali kuhusu kanuni.
Ukisoma biblia kwa ukaribu, umakini na kwa neema utagundua
kuwa mambo mengi sana yameandikwa ndani ya biblia usiposaidiwa na aliyeandika
kuelewa huwezi kuyaelewa kirahisi. Na hasa mengi ambayo Bwana Yesu aliyafundisha
na kusema kwa kinywa chake mwenyewe. Nilipokuwa nasoma na kujifunza, kwa mfano
habari za ufalme wa mbinguni, nikakutana na maneno makubwa mawili, yaani SIRI
na FUNGUO ZA UFALME wa mbinguni. Kwamba mambo mengi ukiyasoma unaweza kushindwa
kuyaelewa kwakuwa ni SIRI,au yamefichwa na ili uijue siri ni lazima ufuate njia
ya kukusaidia kujua hiyo siri. Kikubwa ni kwamba, kuna watu wachache wamepewa
neema au kibali au wamejaaliwa kuzijua hizo siri za ufalme wa mbinguni kama
Mathayo 13:11 inavyosema. Kumbe ukishaijua siri ni wazi kuwa hiyo inaweza ikawa
ndo funguo ya kukusaidia kufungua eneo maalum la maisha yako ambalo lilikuwa
limefungwa na hasa kwenye ufahamu wako. Kumbuka ukikosa maarifa na ufahamu wa
Mungu ndani yako ni wazi kuwa utaishi maisha ya kusumbuka sana. sasa, utaona
hapo kuwa kumbe siri na funguo zimefichwa ndani ya neno la ufalme au neno la
Mungu. Kwahiyo ili uzijue hizo siri na funguo ni lazima ujifunze neno kwa kina.
Hizi siri na funguo, ukishazipata utagundua kuwa zimeficha KANUNI, yaani ukipata
ufunguo unakuwa umefunguliwa ufahamu wako na unapata kitu ambacho ukikitumia
kinakuvusha kwenye mengi lakini kumbuka kuwa funguo ya stoo haifungui mlango wa
chumbani hata kama makufuri yanafanana.
Kwa ndani kabisa ya kila kanuni utagundua kuwa kila kanuni
huwa imeficha au imebeba NIA YA MUNGU. Na hapa naongelea kanuni ndani ya ufalme
wa Mungu. Kwahiyo ukiijua au kuifahamu kanuni ambayo pia ni kweli, basi ujue
umeijua NIA ya Mungu juu ya kanuni husika. Hii inamaansha sasa kuwa, ukisoma
Mathayo 6:1, unaiona kanuni ya jumla kabisa ambayo inaleta picha na kutupa sisi
tunaosoma kujua nia halisi ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kumbuka NENO
NDIO MSINGI WA KANUNI,na hata hivyo NENO ndio kanuni ya msingi. Tuendelee sasa.
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, hapa naambiwa
nini, kama unavyoambiwa wewe. Haisemi usifanye wema lakini kinachoulizwa hapo
ni nia ya kufanya huo wema na unaufanyaje. Hayo ndo maeneo makubwa mawili hapo
ndani. Kufanya wema sio shida, shida ni lengo la kuufanya huo wema, nia ya
kuufanya huo wema na unaufanyaje. Ukiufanya wema wako ili watu wakutazame na
kukusifia na kukupigia magoti ni sawa na kujiharibu wewe mwenyewe. Kwa lugha
nyingine, ukitenda wema ili uonekane kuwa umefanya basi huko kuonekana ndo
kunakuwa thawabu yako na kwa wakti huo huo unakuwa huwezi kupata thawabu
inayotoka mbinguni. Nikifanya wema kwako, kwa lengo la kutaka kuonekana kuwa
hata mimi naweza kufanya au ili nionekane naweza kufanya kuliko wengine au
kwasababu yoyote ya ubinafsi basi thawabu yangu inaishia kwa hao hao watu au
huyo huyo mtu ambaye nimemfanyia. Huyo mtu ataniona mimi kama mkombozi wake,
ataninyenyekea, atanishukuru sana, atanisifia sana jinsi nilivogusa maisha yake
na huku kumbe mimi maisha yangu hayajaguswa na Mungu kwani ndiye mwenye thawabu
ya kweli.
Wema unaofanywa ili kujionyesha unakosa kibali na thawabu
toka kwa Mungu mwenyewe hata kama jambo hilo au tukio hilo litafanikiwa kwa
kiwango gani,kanuni ni ile ile. Nia ya kutenda mema kwa wengine ni Mungu. Ili
Mungu akuone maana yeye ndiye mwenye thawabu na huitoa thawabu kwa kila mtu
anaetenda sawa sawa na kanuni. Ukiisoma kwa undani hii kanuni utagundua ni kama
inakataa majivuno na kiburi, pia inayapinga mashindano na kila namna ya
kujionyesha. Ndo maana inasema ukifanya wema ili uonekane au utazamwe na watu
basi huko kutazamwa ndo kunakuwa thawabu yako na unakosa thawabu ya ukweli toka
kwa Baba yakow a mbinguni.
Angalia mifano ilotolewa, sadaka, maombi, na kufunga
utashangaa sana kama ukiamua kulitazama neno hili kwa jicho la tofauti kidogo.
Najiuliza mbona natoa sadaka sana lakini sipati au sipokei? Mbona naomba san
ahata kama sijui sana maana yake nini? Mbona nafunga sana 3 kavu, 21 na maji
lakini matokeo ya ile thawabu ninayotakiwa kuipata toka kwa baba yangu aonaye
sirini hayalingani wala kufanana? Inaniumiza na kuniboa sana. nikifunga
sitakiwi kufunga kama wanafiki,nisalipo sitakiwi kusali kama wanafiki na hata
nikitoa sadaka nisitoe kama wanafiki maana wao hufanya ili waonekane na watu
kuwa na wao wamo. Ndo maana kumbe mambo mengi tu sijibiwi au siioni ile thawabu
ya kufanya mambo hayo. Kumbe kila nilifanyalo lina thawabu kwa Mungu, ila sasa
kuipata hiyo thawabu ndo mpaka nifuate hiyo kanuni. Hili ni jambo zito.
Nakuombea ukimaliza kusoma usome tena na tena. Umshirikishe na mwingine. Natamani
kutoka hapa moja kwa moja. Unafiki unanitesa sana. ee Mungu nifungue nitoke
kwenye kufanya vitu ili nionekane. Ndo sasa nakaa na kujishangaa, kwani
nimeanza kutenda wema lini? Mpaka nikamkumbuka Kornelio ambaye sadaka zake
zilifika mbinguni na Mungu akamletea msaada wa kuokoka kwani alitoa si kama
mnafiki bali kama mwana wa Mungu.
Najiuliza ninapoandaa matamasha au events za vijana,
ninapoandika jumbe kuwafundisha vijana, je ni kweli nina nia safi au
najichimbia kaburi la mbigiri mimi Raphael? Ninaposhauri au kusaidia, huwa nata
nishukuriwe ndani kwa ndani? Nia yangu ikoje? Ndo najiangalia hapa, je hao watu
wanaotaka kunipa thawabu kwa kunisifia kisa nimetenda wema wao ndio wabaya?
Najiona kabisa. Ujinga wangu uko wazi na upumbavu umefunuliwa hakika. Bwana
Yesu niponye. Wewe jiulize tu, unapofanya CHARITY, unakusanya nguo zako, viatu
na vyakula, unapoimba au unapoandika? Basi itoshe kwa maneno haya kwamba watu
hufanywa wabaya kutegemea na kiwango cha wema kilicho ndani ya mtu. Najiombea
na kukuombea wewe utakaesoma hapa kwamba tufunguliwe na tuwe huru,tutoke kabisa
kwenye udanganyifu wa macho na masikio ya watu ili tupate thawabu ya ukweli
toka kwa baba yetu wa mbinguni,YEHOVA.
By Raphael JL:
0767033300.
Dodoma,Tanzania.
Hakuna maoni: