WARAKA WA PASTOR RAPHAEL JL KWA; Wachungaji na walezi wa vijana, Waimbaji, Wanamuziki na wadau wa muziki


WARAKA WA PASTOR RAPHAEL JL KWA:

Wachungaji na walezi wa vijana Tanzania

Waimbaji

Wanamuziki na wapigaji wa vyombo

Wadau wa muziki

Utangulizi
Kuna mambo kadha ya msingi ambayo waraka huu unaweza kuyaibua na kuyaleta kwenu na kutazamwa kwa jicho lingine ila yote ni kwa ajili ya UTUKUFU WA MUNGU. Waraka huu unaleta kwenu mambo makuu na makubwa yafuatayo ambayo yamejadiliwa kwa kina nab ado kuna fursa ya kusema maoni na hata makaripio au maelekezo ya kiMungu juu ya jambo hili.

1. Ukweli kuhusu wapigaji na waimbaji wa GOSPEL

2. Mjadala kuhusu waimbaji na wapigaji kulipwa kwa huduma yao makanisani

3. Ushauri wa walezi na wachungaji wa vijana

4. Uzuri wa kuifuatisha namna ya dunia hii

5. Ushauri wangu wa jumla.

Kwanza nianze kuwaomba msamaha wale waliokwazika, na hasa wale walioamini kuwa nisingeweza kupost ushauri wa kuwaambia vijana wenye vipaji vyao waende wakavitumie kwa wasioamini kama hawalipwi makanisani kwao. Pia nielezee tu kuwa, ni namna nilivyoamua kutumia fasihi ili kuleta uelewa juu ya jambo hili. Ila kimsingi huo ushauri sio wa kuufanyia kazi hata kama una vitu vya kuviweka sawa na ambavyo vingi pia vimejadiliwa kwenye ukurasa wangu wa FB. 

Mjadala unazidi kushika kasi kutokana na mada yenyewe ambayo ni kama inaogopwa kujadiliwa ingawa pia inawapoteza vijana wengi sana ambao wanakosa maarifa na ufahamu kuhusu jambo lenyewe. Lakini pia ni kwasababu ya uhalisia wa mazingira na ulimwengu tulionao ambao unalazimisha kuishi aina fulani ya maisha ya namna ambayo kama hujakaa vyema unaweza ukajikuta unamuabudu baali.

 Kikubwa sana ambacho ndo kimekuwa gumzo ni uhalali wa wapigaji na waimbaji wa nyimbo za INJILI na hasa wapigaji kutaka kulipwa kama wanavyolipwa wachungaji kwani wote wanafanya huduma. 
Ukweli kuhusu wapigaji na waimbaji wa GOSPEL uko wazi sana maana tunaishi nao na tunaona tabia na mwenendo wao makanisani na tunaweza kusema mengi juu yao. Ila nafasi yao ni muhimu na inajulikana na kutambulika na hili najua liko wazi kwa pande zote. 

Ni watu wenye umuhimu sana kwani muziki kwa ujumla wake una nguvu yake. Hii ina maanisha kwamba makanisa ambayo yamewekeza vizuri kwa vijana wenye vipaji kwenye eneo hili wanaweza wakajikuta wana waumini au washirika wengi kwani watu wanapenda muziki kwa ujumla hata kama ni muziki wa ala au AKAPELA au wenye vyote viwili.

Gumzo kubwa lipo kwenye malipo, yaani kama ni sawa au si sawa kwa kundi hili tunalozungumzia kulipwa au kutokulipwa makanisani ili wasitoke na kwenda kupiga mziki kwa makundi ya muziki ya watu wasioamini au ambao hawajaokoka huku kukiwa na maonyo ya kuharibiwa tabia kama mtu akikaa na watu wenye mazungumzo mabaya au kufungiwa nira pamoja na wasioamini kwa ujumla.

 Kimsingi ili tujue na tuelewe kuhusu swala zima la ulipwaji ni lazima pia tujiulize au tuelewe mambo makubwa mawili:

1. Kipaji changu kinamtumikia nani?

2. Je nimeitwa na nani?

3. Kipaji changu kinamuhudumia nani?

Umuhimu wa maswali haya ni kuwa yanasaidia kujua nani ananilipa na inaniondolea kuwalaumu watu wasiohusika kwani nikitegemea kulipwa na muhudumu badala ya aliyeniita na ambaye kimsingi ndiye ninaemtumikia itakuwa ni hatari kubwa. Ni muhimu pia kujua kuwa, kipaji cha bila mtu wa kumhudumia hakina maana wala thamani. Mfano, kama najua ninaemtumikia ni Mungu basi sitambugudhi mchungaji kunilipa kwani njia ya mchungaji kunilipa inaweza ikawa moja, ila njia ya Mungu kunilipa hazina mipaka. Hii haiondoi wajibu wa kanisa kuwajibika na kuniwezesha kila inapobidi. Kumbuka kuwa ninaemuhudumia ni mtu anaefaidi huduma yangu na sio anaenilipa kimsingi.
Pia katika kulichambua hili ni lazima tuchambue kuwa kuna aina ya wapigaji na waimbaji angalau wa aina mbili kwa sasa. Kuna wale ambao hawana kazi nyingine na wapo kila siku kanisani  na kazi yao ndio huduma yao. Hili kundi linatakiwa litazamwe kwa umakini kwani kama ni kweli kwamba mtu hana kitu kingine cha kufanya kabisa na maisha yake ameyatoa kanisani basi kuna haja ya kanisa kumtazama kwa namna ingine. 

Hii haiondoi kiwango cha yeye kujiuliza ni nani anaemtumikia. Kwa namna yoyote ile inategemea sana na mila na tamaduni zilizojengwa kwa uhalisia wa maisha ya kanisa husika. Hii inanipeleka kwenye kundi la pili na jambo ambalo linahitaji pia kuwa halisi. Kuwa full time mpigaji au mwimbaji haimaanishi mtu unakuwa unapiga au unaimba kila siku, je siku zingine unajishughulisha na nini? Au ndio watu wanaamua kwenda kwa Awilo Longomba kupiga halafu Jumapili wanatokea kanisani au kwenye mazoezi?
Kuna ukweli usiopingika kuwa wapigaji na waimbaji wengi hawapendi kusoma au kufanya kazi, kwa maana ya kazi zingine nje ya kutumia kipaji chake ilia pate pesa. Nimesema wengi, sio wote na utofauti pia unaonekana kwenye kiwango cha malalamiko ambayo yanakuja kwenye jambo hili la kulipwa. Kwa wale wanaojishughulisha na kazi nyingine kwenye maisha yao ni wazi kuwa wanaona maisha yanaenda kwani wana njia nyingine ya kupata kipato. Ni lazima pia kujua kuwa kwa mfumo tulionao kama nchi bado hakuna miundombinu rafiki inayoweza kukufanya utegemee tu kipaji chako kwa njia halali kama hazijaungana na madawa ya kulevya au ushoga na ukapata mafanikio unayoyaota. Ni wachache wamefikia hapa na asilimia kubwa lazima utakuwa amepata watu sahihi wa kumsaidia kupiga hatua.
So ukiangalia ni kama wapigaji wanataka kulipwa, waimbaji wanataka kulipwa na hii inamaanisha kuwa waombaji pia walipwe maana zote ni huduma za muhimu. Mwamko huu unaweza kuwa hatari sana na kutoa mpenyo kwa LUCIFER kuyaharibu makanisa au kuwaharibu vijana wenye vipaji wanaotafuta pesa na hawazipati kanisani. 

Hapa kikubwa kinachotafutwa ni pesa, so mtu anaifuata anakoweza kuipata. Pia kuna tuhuma za baadhi wa wapigaji kukwepa maombi na kutokutulia ndani ya ibada na hasa baada ya wao kupiga huonekana wakitoka nje kupiga stori na kujisifia jinsi walivyovunja. Ipo pia kwamba wengi hawapendi kujifunza au kufundishwa au kuwa chini ya mamlaka ya mtu mwingine. Na hii inanipeleka kwenye pointi yangu ingine kuhusu walezi na wachungaji wa vijana. Ni hatari sana kuwashauri vijana waende huko kwa waperezi kupiga show na kupata hela eti kisa kanisani silipwi. Huu ni uuaji wa wazi. Huu ni uharibifu wa kiwango cha juu sana. Naomba nieleweke hivi.
Swala la kufaidi na kupata faida ya vipaji vyetu liko wazi sana ndani ya biblia n ahata Mungu mwenyewe ameonyesha wazi kuwa anapotufindisha kwa chochote anatufundisha ili tupate faida. Na hata mifano mingi ambayo Bwana Yesu aliitoa kuhusu Ufalme wa Mbinguni aliitoa kwenye mlengo wa faida na ni wazi kuwa lazima tufaidike.

 Mfano mzuri ni swali ambalo Mtume Petro alimuuliza Bwana Yesu kwenye Mathayo 19:27, Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi? Hili jambo sio dogo, ila linawezekana na linaeleweka. Pia kumbuka hawa walikuwa wanaitwa kwenye WITO WA KUACHA NYAVU yaani kuacha kazi zao za awali na kuanza kuwavua watu. Kikubwa ni kuwa kuna namna ya kufaidika ambako Petro alikuwa anaulizia na hasa ukilinganisha na kwamba kuna kazi walikuwa wanafanya kabla. Ukiendelea kusoma utaona sehemu mbili za jibu la Yesu ambazo ni muhimu sana kuziweka kwenye kila tunachokifanya. Kuna kupokea mara mia na kuurithi uzima wa milele, ila cha ajabu ni kwamba hawa Mitume walikufa si katika utajiri wa mara mia ambao ungeonekana kwa macho moja kwa moja na hili linajulikana nai wote.
So kama nikimshauri kijana kwenda kwa kumtumikia Baali maana yake nimekosa suluhisho la kumsaidia ili moyo wake usiharibike kwa kwenda kumuinua mungu badala ya Mungu. Kuna sababu inatumika pia, KOSA LA ANAEKULEA, yaani wengi wamekuwa wanasema watu wa gospel ni wazushi au sio wakweli au wanachelewesha pesa ukifanya nao kazi au wanadunduliza. Huenda wakawepo na wala sikatai, ila kosa langu linakupaje wewe nguvu ya kukosea pia? Mfano kwakuwa wazazi wangu hawakunilea vizuri basi na mimi nimuonyesha kazi binti yangu Favour ili ajue niliteswa pia? Ingawa ninao uhuru wa uchaguzi, yaani kuchagua kujifunza kutoka kwenye makossa hayo na kuwa mwangalifu. Je, mke wako akikukosea unamuacha unaenda kuoa mwingine? Warumi 1:32. Kuunyamazia uovu ni kuukubali. Na hii inanipeleka kwenye pointi ya karibia na mwisho.

Warumi 12:2 inaonyesha kuwa dunia hii au ulimwengu huu una mifumo yake, ina miziki yake, mavazi yake, mfumo wake wa kufikiri, mwenendo wake, mfumo wake wa maisha kwa ujumla na ukifanya kama wao ujue umeamua kuufuatisha na kufana nao. Na kwa upande mwingine wewe unatakiwa kuwa nuru ya ulimwengu, sasa nuru ikifanana na giza si ni giza la hatari hilo? Na kwa upande mwingine wewe unatakiwa kuwa chumvi, na chumvi ikiharibika unairejeshaje? Kwa kiwango gani unaweza kukaa na kufanya kazi na wasioamini nab ado ukabaki uko vizuri na Imani yako isitetereke? Najua wapo wanaoweza ila je ni wangapi kati ya vijana tulionao wanokimbilia kwa Wahiti wanabaki salama? Kama nilivosema hapo juu, kama ni hela tum bona zipo za kutosha mikononi mwa waharibifu na ili kuzipata ni rahisi sana kwani unaamua tu kushusha viwango na kufanana nao.

Na kwa hiyo ushauri wangu wa jumla unafungwa kwenye ukweli kwamba maisha ni uchaguzi wa mtu, yaani aina ya maisha ambayo kila mtu anayaishi anachagua kutegemea ubora wa ufahamu na maarifa aliyonayo ndani yake. Hata leo ukiamua kutembea uchi wala hakuna atakekuzuia, hata ukiamua kuchagua maamuzi yanayokuharibu bado ni maisha yako. Mimi naamini hatma ya kila mtu iko mikononi mwa Mungu. Naamini kuwa MUNGU SIO DIWANI na anaweza kukusaidia kwa njia anazojua yeye ila kama hauko tayari hawezi pia kukulazimisha. Unaweza kujikagua na kujifanyia tathmini, labda kwa wale wanaoenda kupiga au kuimba kwa Wafilisti ni nini kimebadilika ndani ya maisha yao kiroho na kimwili, ni hatua gani wamepiga katika kumjua Mungu Zaidi? Yohana 17:3. Ni kweli mazungumzo mabaya huharibu tabia njema? Mimi binafsi niko tayari kufanya kazi na waimbaji na wapigaji na hata kukutana na kujadili kwa kina maana maandishi yanaweza yasilete majibu ya kila kitu. Na ndio maana nimeandaa kambi ambayo waalimu mbali mbali ninaowaamini watapata nafasi ya kufundisha kuhusu mambo haya mwakani 2017 kwa neema ya Mungu. 

Basi ni vizuri kuona kama kipaji changu hakinitumikishi na wala hakiniharibu maana nilipewa ili nipate faida, yaani nimtumikie aliyenipa nikiwahudumia wanaokihitaji. 

Unaweza kutembelea mafundisho yangu mengi kuhusu KUABUDU kwenye www.fichuka.blogspot.com

Kwa uchache wa mengi.
Pastor Raphael JL:
0767033300
DODOMA.

Maoni

Chapisha Maoni