MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU
31.12.2016
MAANDALIO YA MOYO NI YA MWANADAMU-PLAN 7.21
Mithali 16:1-3
“Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana. Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; bali Bwana huzipima roho za watu. Mkabidhi Bwana njia zako, na mawazo yako yatathibitika”
Leo ni tareh 31.12.2016, ndo siku ya mwisho ya mwaka 2016 na kama unasoma hapa basi inamaanisha umepewa maisha ya kufika siku hii ya mwisho kabisa kwa mwaka huu. HONGERA SANA. Najua ulipanga mengi kwa mwaka huu na sina hakika ni mangapi ulifanikiwa bila kushusha viwango au kulegeza kanuni. Mshukuru Mungu hata kwa machache ulofanikiwa kuyafanya, kwa afya ulonayo na wema wake kwako kwamba hajakutoa kuwa mawindo kwa adui zako. Leo naandika post hii ya mwisho kwa mwaka huu 2016 ili kukutia moyo, hata mimi mwenyewe sijatimiza kila kitu nilichopanga kwa mwaka huu ila robo tatu nimefanikisha kwa neema ya Mungu. Karibu tumalizie mwaka huu kwa tafakari hii ya MAANDALIO YA MOYO NI YAKO.
Nianze kwa kusema hivi MAN PURPOSES, GOD DISPOSES kwa maana ile ile ya kwamba dhamiri au nia isiyoongozwa na neno la Mungu inakuwa kipofu. Yaani ni wajibu wangu kupanga au kukusudia jambo lakini ni Mungu ndiye anaeruhusu lile nililokusudia kuja kuonekana na kuwa halisi kwa namna ambayo bila Mungu mipango yangu haina uzima ndani yake. Mwanadamu anakusudia, Mungu anadhihirisha, hili ni la msingi sana kulielewa na ndio maana maandalio ya moyo ni yako wewe kama mwanadamu lakini jawabu linatoka kwa Mungu. Kwa lugha ingine, ni muhimu kwa na maandalio ya moyo, kuwa na mipango au kukusudia mambo ila tujue kuwa jawabu hatunalo sisi kama wanadamu, jawabu la hayo yote tunayopanga linatoka kwa Mungu.
Au lugha nyepesi ya kingereza niseme WE CAN MAKE OUR PLANS, BUT FINAL OUTCOME IS FROM GOD. Tunaweza kuweka mipango yetu lakini jawabu la mwisho la mipango yetu linatoka kwa Mungu. Ni muhimu kujua kuwa Mungu peke yake ndo anajua nini kitatokea kwenye maisha yetu kila saa ya kila siku ya mwaka 2017 na kwahiyo ni muhimu kumpa heshima yake pia. Kikubwa ninachotaka kukionyesha hapo ni kwamba IT IS EASY TO RATIONALIZE ANYTHING WITHOUT ESTABLISHED STANDARDS. Yaani, katika umahiri wetu wa kisomi, wa kiufahamu na kiubinadamu wenye ubinafsi wa kutosha ni rahisi sana kutafuta maana na hata kutoa thamani ya mambo tunayofanya kwa kila kitu ili mradi tu hatuna KANUNI inayotuongoza. Ndio maana njio zote za mtu ni safi machoni pake lakini Bwana hupima sio tu njia bali kule ambako njia hizo zinatoka.
Jingine kubwa la kujua ni kuwa Mungu anataka kukutumia kwa kutumia UFAHAMU wako au kwa ufahamu ulionao. Ni wazi kuwa mwaka 2017 kama Mungu ataokoa watu, kama ataponya au kama atafufua au kama atawatia moyo watu ni lazima afanye hivo kwa kutumia watu walio tayari na huenda moja kati ya watu waliotayari ni wewe maana kuwa tayari kutumiwa na Mungu ni maamuzi yako. Mungu hawezi kukulazimisha kukutumia kama hauko tayari na atakutumia kwa kiwango cha ufahamu wako, yaani kama hujasoma atakutumia hivohivo, kama umesoma atakutumia hivohivo, kama ni masikini atakutumia tu kuwafikia wenzako na kama ni tajiri atakutumia tu. Ndani ya ufahamu wako ndiko kwenye mawazo na fikra zako, na hizo ndio mipango yako. Ila hii mipango yako ni lazima ipate kibali mbele za Mungu ili iweze kulitumikia kusudi kubwa la Mungu zaidi tu ya kukufanya wewe ni kuwa mtu mkubwa sana.
Weka akilini mwako kuwa KIWANGO CHA UTUKUFU WA MUNGU ULICHOKIBEBA NDIO KITATUMIKA KUKUTUKUZA kwa kila jambo utakalolifanya kwa ajili ya Mungu. Yaani, ukifanya jambo la Mungu mahali Mungu atakusifu kwa kadri ya sifa ulizomletea. Unaposema unafanya jambo kwa ajili ya utukufu wa Mungu unatakiwa umaanishe kuwa ujambo unalofanya litamtukuza Mungu na litafanya Mungu azidi kujulikana zaidi kupitia hilo na kadri anavyojulikana na kufahamika na kutukuzwa na wewe uliefanya jambo hilo ujue unakula humo humo ndani. Ndo maana mpaka leo kuna watu bado wanasema MUNGU WA ELIYA, kwani wao bado hawajmdhihirisha Mungu wao kwa kiwango cha Eliya na wanabaki na mfano huo maana hawana mwingine. Mungu atanitumia mimi kama Raphael na sio kwa utukufu wa Samwel Sasali kwani kila mmoja wetu ana PIPA LAKE LA UTUKUFU lilifungwa ndani ya kusudi lake.
Usisahau kuwa upo mtego kwani njia zako zote unaweza kuziona ni safi na ni sawa lakini kumbe huo ndio ukawa uharibifu wako, kumbuka uharibifu una kifurushi chake, yaani ukijiharibu unaharibu vingi pamoja na wale wanaokuamini pia. Kwakuwa sisi kama wanadamu kwakweli hatuamini kihivyo sana maana hata mioyo yetu amabyo ndio inafanya maandalizi Yeremia anasema moyo ni mdanganyifu na una ugonjwa wa kufisha. Kwakuwa hivo ndivyo ilivyo basi ndo maana leo nakusihi popote ulipo MKABIDHI BWANA KAZI ZAKO ILI MAWAZO YAKO YATHIBITIKE. Hii inamaanisha unaingia kwenye makubaliano ya kutembea na kufanya kazi na Mungu. Kazi ni kwako mwenyewe. Maamuzi ni yako pia.
Kumkabidhi Bwana kazi zako haiwezekani mpaka uwe umeamua kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwani huwezi kumkabidhi kazi ambazo unajua kabisa hazikubali. Inawezekana kabisa kuwa hata mwizi anamuomba Mungu ila najua sio Mungu labda awe mungu. Pata muda wa kumkabidhi kwa kutaja kila kazi yako ya 2017, aiandike mahali halafu msomee Baba yako wa Mbinguni. Ngoja nielezee kidogo hapa. Unaweza kukabidhi kazi yako kwa Mungu ili kutimiza wajibu, mimi siongelei hii maana hii ni sawa na kutaka kumdanganya Mungu kwa kumpa pipi. Halafu unaweza kumkabidhi Bwana kazi zako na ukaishia kuzifanya mwenyewe na sio Bwana kukusaidia kuzifanya kwa ushahidi wa nguvu zake. Mimi namaanisha kumkabidhi kazi zako na wewe kusimama kwenye nafasi yako kufanya kwa kusikiliza na kufuata maelekezo yake. Kumbuka yeye ndo mwenye jibu lake.
Unapopanga kwa ajili ya mwaka 2017 hebu jiulize maswali haya matano:
1. Huu mpango au hii mipango imetoka wapi au chanzo chake ni nini?
2. Je, mpango huu au mipango hii iko sawa na au inaendana na KWELI YA MUNGU?
3. Je, inatekelezeka au inaweza kufanya kazi kwa kuangalia mazingira halisi ya kimaisha iliyopo sasa?
4. Je, CHUJIO langu au mtazamo nilionao unampendeza Mungu kwa kiwango gani juu ya mipango yangu yote?
5. Nini kusudio la mwisho au kwanini umepanga hayo yote, hatma ya mipango yako ni nini mwisho wa siku na hasa baada ya kufanikiwa?
Hakikisha una jibu hayo maswali yote kwa uhalisia. Ukihitaji shahidi wa mipango yako ya 2017 basi lete mipango yako kwa namba yangu whatsapp tu 0767033300. Mungu akubarikie na kukustawisha mwaka 2017. IMARISHA USHIRIKA NA YEYE.
By Pastor Raphael JL:
Founder of YKM, EFs, GP na CWP.
Box 3613-Dodoma.
Mungu Kwanza 2016.
Hakuna maoni: