LULU ILOFICHWA SHAMBANI: NGUVU YA MAZINGIRA SAHIHI
05.01.2015
LULU ILOFICHWA SHAMBANI: NGUVU YA MAZINGIRA SAHIHI
Jesus Up!
Mungu alipomaliza kuumba kila kitu alimuumba Adam na kumuweka ndani ya bustani ya eden, mazingira hayo ndo yalikuwa mazingira sahihi kwa Adam kuweza kuishi na kutimiza wajibu wake wa kuilima na kuitunza bustani. Kabla hata mwanamke hajaja, Adam alikuwa na uwezo mkubwa sana alopewa na Mungu wa kufanya yampasayo. Ukisoma Mwanzo 2:20, utaona kuwa pamoja na kuilima na kuitunza bustani (Mwanzo 2:15) Adam alipewa uwezo wa kuwataja au kuwapa majina wanyama na wadudu na kila kiumbe kilichoumbwa na Bwana Mungu na cha kushangaza ni kuwa jina ambalo Adam alitoa kwa mdudu au mnyama husika ndo likawa jina lake hata leo hii. huu ni uwezo mkubwa sana wa kubuni au kutengeneza kitu. Usichukulia jambo hili kwa urahisi. Fikiria wanyama wote na wadudu unaowajua na usio wajua mpaka sasa walioko duniani, majina yao walipewa na Adam, huu ni uwezo mkubwa sana.
Naufananisha uwezo huu wa kuumba na kutengeneza vitu ambao Mungu ameuweka ndani ya mwanadamu kama LULU ILIYOFICHWA SHAMBANI. Huo uwezo ni kama lulu, ambayo ili iweze kukusaidia kwa mwaka huu 2016 ni lazima uivumbue, uing’amue na kuitoa mafichoni na kuileta katika eneo la kazi. Shamba nalifananisha na maisha ambayo kila mtu amekuwa nayo, yaani makuzi na malezi ya mtu ambayo hutumika sana kuficha LULU yaani ule uwezo ambao mtu kapewa na Mungu ili autumie atakapozaliwa na kuwa mkubwa. Utaona kuwa Adam alipewa hiyo lulu, ule uwezo ulikuwa ndani yake yeye, hatuoni akienda kuuazima mahala au kuununua tena au kuigilizia bali tunaona ule uwezo wake unatokea ndani yake na akafanya kwa kadri ya uwezo wake. Akawapa majina wanyama na wadudu wote mpaka leo. Kuna mambo ya kujifunza kwa kuangalia uwezo nah ii lulu ilokuwa imefichwa ndani ya Adam na hasa ukizingatia kuwa leo ni siku ya tano tu ya mwaka 2016 kwa hiyo bado na wewe unaweza KUJITAFUTA ili UJIFICHUE na kuitoa ile lulu shambani.
Kwanza tufahamu kuwa ni Mungu ndiye anaetupa uwezo huo, yaani ile lulu imetoka kwa Mungu kama alivyompa Adam. Mimi na wewe kwa mwaka huu mpya tunatakiwa kutambua kuwa tunao uwezo mkubwa sana ndani yetu ila ipo changamoto. Jambo la pili ndo changamoto, wakati kwa Adam uwezo wake ulopewa ulikutana na mazingira sahihi yaliyomuwezesha kuutoa ule uwezo na kuingiza katika utendaji na kazi kuonekana mpaka leo, makuzi na malezi ya Adam yalikuwa sahihi kwa kiwango ambacho uwezo wake ulipata mazingira sahihi. Sisi wengine, tumezaliwa na uwezo, vipaji vingi tu vizuri lakini makuzi na malezi yetu, yaani shamba la maisha yetu limekuwa na visiki, magugu kwa kiwango ambacho ukifanikiwa kujua uwezo wako unakuwa muujiza maana maisha magumu au ya starehe yameharibu uwezo wetu wa kuvumbua lulu.
Kwa namna moja au nyingine unaweza kushangaa sana kwamba, mtu anakuwa omba omba lakini ndani yake anamiliki mgodi wa tanzanite. Mtu anakuwa omba omba lakini ndani yake amejaa vitabu na nyimbo na ubunifu wa mambo. Mtu anailalamikia serikali au wazazi wake lakini kwakweli ndani yake amejaa uwezo wa ushawishi ambao unaweza kumuinua mpaka juu yam lima mrefu kuliko yote Afrika. Hiki ni kitendawili cha tajiri masikini. Mazingira sahihi ndiyo tu yanaweza kukufanya uweze kufanikiwa katika kila jambo hapa duniani na hivo ni lazima ujue mazingira sahihi kwako ni yapi. Nitakwambia mazingira sahihi ambayo ni ya lazima kwa kila mtu au kila kijana ambayo huwezi kuyakwepa kama unataka ile lulu yako iwe na maana na nguvu.
Kwa Adam, mazingira sahihi hayakuwa tu kuwepo ndani ya eneo la kijiografia la eden bali ile kufunikwa na UWEPO WA MUNGU kwa ujumla ndo yalikuwa mazingira sahihi kabisa. Yaani, kimwili alikuwa eneo sahihi na pia kiroho alikuwa kwenye mazingira sahihi pia lakini lazima ujue kuwa UWEPO WA MUNGU una nguvu kuliko mazingira ya kimwili ambayo ndo mfano wa shamba. Yaani unaweza ukawa ulikulia kwenye mazingira magumu sana ya kimwili lakini siku unakaa tu kwenye mazingira sahihi ya kiroho ndani ya UWEPO WA MUNGU basi mambomengi yanaanza kurudi kwenye msitari wake. Adam aliweza kufanya kwa ufanisi kwakuwa alikuwa kwenye mazingira sahihi ya UWEPO WA MUNGU. Mungu akufungue macho yako unaposoma maneno haya. Mungu akusaidie kuona. Mungu akufichulie ile lulu ndani yako.
Jiulize, ni nini kimeficha lulu yako? Fichua. Jitafute. Jikague. Jiulize. Jivumbue upya. Nataka ufahamu kuwa kila uwezo aliokupa Mungu alikupa ili uweze kuutumia duniani na sio baada ya kufa. Yaani baada ya kufa huwezi kutumia lulu yako kwa jinsi yoyote ile maana ukifa unaenda kuishi maisha ya kanuni ambayo wewe hutakuwa na mamlaka ten ahata ya kutumia utashi wako. Ni hapa duniani tu ndo unaweza ukatumia uwezo wako na kuleta mabadiliko, nakusihi kwa jina la Yesu Kristo kuwa maneno haya yasiondoke ndani yako bali yapige kelele mpaka ununue shamba ili mradi umeiona lulu iko ndani yake.
Mungu kwanza, ndo maana nimekuwa nasema hapo ndo mahali pa kuanzia maana ni Mungu huyuhuyu aliyekupa uwezo huo ili uutumie kwa utukufu wake na sio kuuchezea kwa dhambi na starehe. Uwezo wako uliopewa na Mungu ni HAZINA ILIYOSITIRIKA KATIKA SHAMBA, ambayo akiiona mtu mwingine kabla yako basi atakuwa tayari kukununua na kukutumia vile apendavyo na akishamaliza kukutumia anakuacha unaendelea na maisha yako ya kuomba omba na kwa hakika wewe ulikuwa bilionare. Ndio maana ni lazima uhakikishe umetengeneza mazingira mazuri ndani yako ili UWEPO WA MUNGU uweze kukufaa na kukuvumbulia kila uwezo ulio ndani yako. Ni kama nchi yetu, Tanzania, umasikini tunajitakia. Kuomba omba misaada nje ya nchi pia tunajitakia wakati tunazo hazina na lulu, tunayo madini, mafuta, gesi na kikubwa tunao watu, tunayo amani. Mungu atupe nini, MAJIVU YA MKAA?
Mwaka huu wa 2016 ni mwaka wa kumtanguliza Mungu kwanza kama unataka kuvuka kwa salama na kama untaka itakapofika mwezi wa kumi na mbili uweze kuwa na mambo kadhaa ya kumshukuru Mungu. Uwepo wa Mungu katika kila sekunde katika maisha yako ni wa lazima na muhimu sana. Anza leo kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, endelea kuishi katika mahusiano bora na Mungu kupitia Roho Mtakatifu na endelea kuimarisha ushirika na mbinguni. Najua kuwa, kila atakaemaanisha kuingiza ujumbe huu katika utekelezaji lazima ataibuka na shuhuda za kutosha na mimi nangojea kumshukuru Mungu pamoja na wewe.
Inawezekana kabisa kuwa wewe una miliki makampuni kadhaa lakini yamefichwa shambani. Inawezekana kabisa kuwa wewe una vitabu mia na zaidi lakini uwezo huo umefichwa na maisha uloishi. Kwa vyovyote vile, namuomba Mungu kwamba utafunguka na kufunguliwa toka katika kila kufungo kinachokuficha. Ufunguke kwa jina la Yesu na uweze kuona utajiri wa uwezo ambao Mungu amekupa ndani yako. Usisahau, MUNGU KWANZA.
By Raphael JL: YKM Founder
Box 3613.
Dodoma
www.raphaellyela.co.tz
www.fichuka.blogspot.com
Hakuna maoni: