Ads Top

UBAYA WA WATU UKO NDANI YA MTU


October 4, 2016

UBAYA WA WATU UKO NDANI YA MTU

Ubaya ulio ndani ya mtu una nguvu na uwezo wa kuambukiza namna hiyohiyo ya kuwaona hata watu wengine kuwa ni wabaya. Ni sawa na kusema, mganga wa kienyeji hachelewi kuwaona wengine wote pia kuwa ni waganga ila yeye amewazidi uwezo au nguvu. Ni rahisi sana kwa mwizi kuwaona na wengine ni kama yeye maana uzuri au ubaya unaanzia ndani ya mtu husika. Mwanaume asiye mwaminifu kwa mkewe ni rahisi sana kuona kuwa hata mkewe pia hajatulia kama yeye. Hii ni kanuni,ubaya wa watu uko ndani ya mtu kwanza kabla haujatoka nje. Cha ajabu ni kwamba namna hii ya mfumo wa kufikiri mara nyingi hutokea kwa upande wa mambo mabaya na sio mazuri. Kwa mfano ni vigumu sana kwa mtu wa kawaida kuwaona wengine ni waaminifu eti tu kwa sababu yeye ni mwaminifu. Ni wazi pia kuwa HUWEZI KUTOA USICHOKUWA NACHO, ila inategemea sana ulichonacho ni nini na kina ubora wa namna gani. Basi leo tuitazame kanuni hii kwa undani kama Neno la Mungu linavyotufunulia siri hii.
Mathayo 6:1-18.
Kuna mambo matatu yameandikwa ndani ya mistari hii, ambayo yamejengwa kwenye kanuni moja kubwa sana. kanuni hii imenichangamotisha sana na kunifanya niwaze na kujikagua na kujipima na kujiona kama nikipimwa nitakuwa kwenye mizani ipi. Kanuni yenyewe inasema hivi, angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Mathayo 6:1

Ukisoma kwa kuendelea hapo chini mapaka msitari wa 18, utaona mambo matatu yaliyotajwa moja kwa moja yayakiunganishwa na kanuni yenyewe ambayo imetaja WEMA kwa ujumla wake. Na hapo kufanya wema inaweza ikawa inaeleweka kwa namna nyingi sana maana ni jumla ya kila aina ya mambo unayotaka au kutamani kuyafanya kwa watu hata kama ni kuwapa msaada, au kuwashauri au kuwatia moyo au vyovyote vile unaweza kuiweka hapo. kikubwa ni kujua kuwa yako mambo ambayo kanuni imeyabeba na ambayo ndiyo hasa msingi wa somo hili la leo. Niseme machache kwanza kabla sijafika mbali kuhusu kanuni.
Ukisoma biblia kwa ukaribu, umakini na kwa neema utagundua kuwa mambo mengi sana yameandikwa ndani ya biblia usiposaidiwa na aliyeandika kuelewa huwezi kuyaelewa kirahisi. Na hasa mengi ambayo Bwana Yesu aliyafundisha na kusema kwa kinywa chake mwenyewe. Nilipokuwa nasoma na kujifunza, kwa mfano habari za ufalme wa mbinguni, nikakutana na maneno makubwa mawili, yaani SIRI na FUNGUO ZA UFALME wa mbinguni. Kwamba mambo mengi ukiyasoma unaweza kushindwa kuyaelewa kwakuwa ni SIRI,au yamefichwa na ili uijue siri ni lazima ufuate njia ya kukusaidia kujua hiyo siri. Kikubwa ni kwamba, kuna watu wachache wamepewa neema au kibali au wamejaaliwa kuzijua hizo siri za ufalme wa mbinguni kama Mathayo 13:11 inavyosema. Kumbe ukishaijua siri ni wazi kuwa hiyo inaweza ikawa ndo funguo ya kukusaidia kufungua eneo maalum la maisha yako ambalo lilikuwa limefungwa na hasa kwenye ufahamu wako. Kumbuka ukikosa maarifa na ufahamu wa Mungu ndani yako ni wazi kuwa utaishi maisha ya kusumbuka sana. sasa, utaona hapo kuwa kumbe siri na funguo zimefichwa ndani ya neno la ufalme au neno la Mungu. Kwahiyo ili uzijue hizo siri na funguo ni lazima ujifunze neno kwa kina. Hizi siri na funguo, ukishazipata utagundua kuwa zimeficha KANUNI, yaani ukipata ufunguo unakuwa umefunguliwa ufahamu wako na unapata kitu ambacho ukikitumia kinakuvusha kwenye mengi lakini kumbuka kuwa funguo ya stoo haifungui mlango wa chumbani hata kama makufuri yanafanana.
Kwa ndani kabisa ya kila kanuni utagundua kuwa kila kanuni huwa imeficha au imebeba NIA YA MUNGU. Na hapa naongelea kanuni ndani ya ufalme wa Mungu. Kwahiyo ukiijua au kuifahamu kanuni ambayo pia ni kweli, basi ujue umeijua NIA ya Mungu juu ya kanuni husika. Hii inamaansha sasa kuwa, ukisoma Mathayo 6:1, unaiona kanuni ya jumla kabisa ambayo inaleta picha na kutupa sisi tunaosoma kujua nia halisi ya Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu, kumbuka NENO NDIO MSINGI WA KANUNI,na hata hivyo NENO ndio kanuni ya msingi. Tuendelee sasa.
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, hapa naambiwa nini, kama unavyoambiwa wewe. Haisemi usifanye wema lakini kinachoulizwa hapo ni nia ya kufanya huo wema na unaufanyaje. Hayo ndo maeneo makubwa mawili hapo ndani. Kufanya wema sio shida, shida ni lengo la kuufanya huo wema, nia ya kuufanya huo wema na unaufanyaje. Ukiufanya wema wako ili watu wakutazame na kukusifia na kukupigia magoti ni sawa na kujiharibu wewe mwenyewe. Kwa lugha nyingine, ukitenda wema ili uonekane kuwa umefanya basi huko kuonekana ndo kunakuwa thawabu yako na kwa wakti huo huo unakuwa huwezi kupata thawabu inayotoka mbinguni. Nikifanya wema kwako, kwa lengo la kutaka kuonekana kuwa hata mimi naweza kufanya au ili nionekane naweza kufanya kuliko wengine au kwasababu yoyote ya ubinafsi basi thawabu yangu inaishia kwa hao hao watu au huyo huyo mtu ambaye nimemfanyia. Huyo mtu ataniona mimi kama mkombozi wake, ataninyenyekea, atanishukuru sana, atanisifia sana jinsi nilivogusa maisha yake na huku kumbe mimi maisha yangu hayajaguswa na Mungu kwani ndiye mwenye thawabu ya kweli.

Wema unaofanywa ili kujionyesha unakosa kibali na thawabu toka kwa Mungu mwenyewe hata kama jambo hilo au tukio hilo litafanikiwa kwa kiwango gani,kanuni ni ile ile. Nia ya kutenda mema kwa wengine ni Mungu. Ili Mungu akuone maana yeye ndiye mwenye thawabu na huitoa thawabu kwa kila mtu anaetenda sawa sawa na kanuni. Ukiisoma kwa undani hii kanuni utagundua ni kama inakataa majivuno na kiburi, pia inayapinga mashindano na kila namna ya kujionyesha. Ndo maana inasema ukifanya wema ili uonekane au utazamwe na watu basi huko kutazamwa ndo kunakuwa thawabu yako na unakosa thawabu ya ukweli toka kwa Baba yakow a mbinguni.

Angalia mifano ilotolewa, sadaka, maombi, na kufunga utashangaa sana kama ukiamua kulitazama neno hili kwa jicho la tofauti kidogo. Najiuliza mbona natoa sadaka sana lakini sipati au sipokei? Mbona naomba san ahata kama sijui sana maana yake nini? Mbona nafunga sana 3 kavu, 21 na maji lakini matokeo ya ile thawabu ninayotakiwa kuipata toka kwa baba yangu aonaye sirini hayalingani wala kufanana? Inaniumiza na kuniboa sana. nikifunga sitakiwi kufunga kama wanafiki,nisalipo sitakiwi kusali kama wanafiki na hata nikitoa sadaka nisitoe kama wanafiki maana wao hufanya ili waonekane na watu kuwa na wao wamo. Ndo maana kumbe mambo mengi tu sijibiwi au siioni ile thawabu ya kufanya mambo hayo. Kumbe kila nilifanyalo lina thawabu kwa Mungu, ila sasa kuipata hiyo thawabu ndo mpaka nifuate hiyo kanuni. Hili ni jambo zito. Nakuombea ukimaliza kusoma usome tena na tena. Umshirikishe na mwingine. Natamani kutoka hapa moja kwa moja. Unafiki unanitesa sana. ee Mungu nifungue nitoke kwenye kufanya vitu ili nionekane. Ndo sasa nakaa na kujishangaa, kwani nimeanza kutenda wema lini? Mpaka nikamkumbuka Kornelio ambaye sadaka zake zilifika mbinguni na Mungu akamletea msaada wa kuokoka kwani alitoa si kama mnafiki bali kama mwana wa Mungu.

Najiuliza ninapoandaa matamasha au events za vijana, ninapoandika jumbe kuwafundisha vijana, je ni kweli nina nia safi au najichimbia kaburi la mbigiri mimi Raphael? Ninaposhauri au kusaidia, huwa nata nishukuriwe ndani kwa ndani? Nia yangu ikoje? Ndo najiangalia hapa, je hao watu wanaotaka kunipa thawabu kwa kunisifia kisa nimetenda wema wao ndio wabaya? Najiona kabisa. Ujinga wangu uko wazi na upumbavu umefunuliwa hakika. Bwana Yesu niponye. Wewe jiulize tu, unapofanya CHARITY, unakusanya nguo zako, viatu na vyakula, unapoimba au unapoandika? Basi itoshe kwa maneno haya kwamba watu hufanywa wabaya kutegemea na kiwango cha wema kilicho ndani ya mtu. Najiombea na kukuombea wewe utakaesoma hapa kwamba tufunguliwe na tuwe huru,tutoke kabisa kwenye udanganyifu wa macho na masikio ya watu ili tupate thawabu ya ukweli toka kwa baba yetu wa mbinguni,YEHOVA.

By Raphael JL:
0767033300.
Dodoma,Tanzania.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.