Ads Top

KAMA ROHO YAKO IFANIKIWAVYO



24.08.2017
KAMA ROHO YAKO IFANIKIWAVYO

3 Yohana 2
Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.

Nianze kwa kutafsiri hili neno: BARAKA:
Baraka ni jumla ya mambo yote mazuri katika maisha ya mtu, yaani neema, fanaka na mafanikio.


Hata kwa tafsiri hiyo inaonyesha wazi kabisa kuwa Baraka imehusianishwa na mafanikio na ni kama mtu akifanikiwa anakuwa amebarikiwa. Ila pia inaonyesha wazi kabisa kuwa Baraka zinaanzia ndani kwenda nje na sio nje kwenda ndani. Hata kwenye andiko letu, mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo. Ukisoma hiyo vizuri utaona ni wazi kwamba kipimo cha mafanikio ni roho. Roho inaanza kufanikiwa kwanza na ndipo maeneo mengine yote yanaambukizwa yale mafanikio mpaka yanatokeza kwa nje kwa kiwango ambacho aliyebarikiwa anafanyika Baraka kwani Baraka zake ni thabiti.

Warumi 11:29
Karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.


Kwa ujumla wake, chochote anachokupa Mungu hakina majuto, yaani huwezi ukafika mahali ukasema najuta kubarikiwa na Mungu kwani vyote vinavyotoka kwake havina hayo majuto. Mungu akikupa karama haiambatani na majuto. Mungu akikuita huwezi kujuta. Mungu akikubariki huwezi kujuta. Kumbe kujuta ni ishara kwamba Mungu hayupo hapo au hayupo kwenye hilo au katikati ya hilo. Majuto ni ishara mbaya ya mafanikio yoyote. Kwamba kama nimefanikiwa lakini kwa ndani kabisa kuna majuto na kuna namna siko huru au naishi kwa masharti ya kutumia Baraka zenyewe kwa kiwango hata cha kuharibu utu wangu ni hatari sana. 


Jumapili ilopita nilifundishwa kitu kanisani na Dr Ipyana, aliyekuwa anafundisha kuhusu UTOAJI na akakazia Zaidi kwenye ZAKA. Katika mengi aliyofundisha mimi nilimwelewa, katika hayo mengi eneo moja la kutafsiri neno Baraka. Kwamba kwa watu wengi Baraka ni kumiliki vitu vinavyoonekana tu au mafanikio ya vitu lakini ki ukweli Baraka ni Zaidi ya hayo. Unaweza ukawa huna magari lakini bado ukawa umebarikiwa kwani Baraka za Mungu au kubarikiwa na Mungu hakuhusiani na kumiliki vitu maana kama ni vitu hata mataifa wanavyo sana tena kwa njia mbaya. Lazima kuwe na kikubwa Zaidi ya hayo yote. Akiwa anaendelea kufundisha nikadaka kuwa kumbe kubarikiwa na Mungu ni kitu kikubwa sana kwa kiwango kwamba ukijiminya kwenye vitu vinavyoonekana tu unajipunja.


Mungu akikubariki, mfano Mithali 10:6a inasema Baraka humkalia mwenye haki kichwani, huwa nikiusoma  huu msitari najiuliza mengi sana. Baraka hukaa kichwani, na chochote kinachokaa kichwani maana yake kina nguvu na ushawishi mkubwa kwa yule kinaemkalia. Hapo ndo nikagundua kuwa kumbe Baraka ni za rohoni, yaani Baraka zinaanzia rohoni na kutoka nje. Baraka ni roho ya kibali juu ya mtu. Mtu aliyebarikiwa na Mungu ni mtu mwenye kibali, yaani mtu aliyeruhusiwa kufanikiwa kila aendako na kwa kila afanyacho.


Nakumbuka Mungu akamwambia Ibrahim kuwa yeye amebarikiwa, na mtu yoyote atakaembariki basin aye atabarikiwa na yoyote atakemlaani basi amelaaniwa. Mtu aliyebarikiwa na Mungu halaaniki. Haepukiki kufanikiwa. Hazuiliki. Unzuilikable. Unpingikable. Unkwepable. Unkimbilikable, kimsingi kumfukuza mtu aliyebarikiwa na Mungu ni kuzifukuza Baraka, kumkataa mtu wa namna hii ni kuzikataa Baraka ambazo ziko juu ya kichwa chake. Yaani mtu aliyebarikiwa amefunikwa na kibali cha ruhusa ya kufanikiwa yeye na kuwafanikisha wengine wote ambao watamkubali. Hakika kubarikiwa na Mungu ni jambo jema na zuri sana. Mtu aliyebarikiwa ni Baraka popote maana anajua nafasi yake kwa Mungu na anasimamia zile kanuni zilizompa Baraka.


Mtazamo huu ni tofauti sana na kile kinachoonekana duniani. Kwamba Baraka ni kumiliki mali na utajiri. Wala sisemi kuwa tajiri ni vibaya, ila nasema mali na utajiri ni matokeo na sio hatma. Mfano kuwa tayari kuiba au kusema uongo au kuua ili tu uwe na mali au ili uonekane na wewe umebarikiwa ni mateso sana. Kufanya uasherati na uzinzi ili upate kazi au biashara ifanikiwe kwa rushwa haya ni mateso makubwa sana. Ndio tunaona udanganyifu wa sasa, watu watapiga picha nyuma kuna magari au majumba mazuri yenye ramani nzuri ili kuwavutia watu watafsiri mafaniko na Baraka kwa jinsi hiyo na tumeona wengi sana wakiharibika.

Kanuni ni ile ile KAMA ROHO YAKO IFANIKIWAVYO,je kufanikiwa kwa roho ni kupi? Naomba tuendelee kujifunza na kama utakuwa umepata kitu au uelewa wa roho yako inavyofanikiwa basi tufundishane. Naogopa sana mtu anaenishikisha sana magari, manyumba na pesa kuliko Mungu katika Kristo.

By Raphael JL
0787110003
www.fichuka.blogspot.com

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.