Ads Top

HUWA UNAMKUMBUKA IKIWAJE???



23.12.2017

Huwa unamkumbuka ikiwaje? Au nini kikitokea au ukisikia na kuona nini au ukimuona nani? Au ukienda wapi na ukakutana na nini? Au ukipita kwenye hali gani, ugumu au wepesi? Huwa unamkumbuka nani? Ukisikia umbea na majungu na uongo na hila na mambo ya hovyo hovyo huwa unamkubuka nani? Ukisikia mambo mazuri na ya kujenga huwa nani anakuja kwenye ufahamu wa moyo wako? Lazima kuna mtu huwa unamkumbuka mambo fulani hivi yakitokea.

Huyo unaemkumbuka ndio yuko kwenye kiwango na ubora wa jambo lililotokea mpaka ukamkumbuka. Yaani, kuna watu tunawakumbuka tu ukisikia maneno fulani hivi matamu na wengine ukisikia maneno fulani hivi machungu. Kuna watu tunawakumbuka tukiwa na shida zetu za kututosha maana wao ndio kimbilio hata kama baada ya kutusaidia huwa tunawatupilia mbali hata kuwasalimia. Kuna watu huwa tunawakumbuka tukiona wanyama kwani wana tabia zinazofanana nao. Ukimuona chiriku unaanza kumkumbuka tu jamaa anayefanana nae.

Wewe huwa unakumbukwa kwa maneno gani au tabia gani au picha gani au mnyama gani? Ukikumbukwa unatafutwa hapo hapo. Ukikumbuka unamtafuta hapo hapo. Nini ni ishara na alama yako kwa watu. Unakumbukwaje? Kwa uongo au uzinzi au tamaa au uzushi au maneno yasiomaana au kwa lipi? Ni rahisi sana kujua unakumbukwaje na wengine kama hkuishi maisha ya unafiki. Kumbuka ulivyokuwa unaishi nao, unaongea nao, unavaa, unalala maana hata kukoroma kunaweza kukufanya uwe unakumbukwa tu.

Kuna watu tumetunza namba zao kutokana na umuhimu wao kwetu hata kama hatuwasiliani nao mara kwa mara. Kuna watu huwa tunaanza kutafuta mawasiliano yao baada ya jambo fulani kutokea. Kuna watu hata iweje huwezi kuwapotezea. Kuna watu wakipiga simu au kuandika ujumbe lazima tuwaulize wao ni akina nani. Maana tuliachanaje? Tuliishije? Ndo maana unaona leo, yule ambaye ulikuwa unamuona kama si kitu ndo ameketishwa pamoja na wakuu na kinakuuma sana kwamba kwanini hakukumbuki. Mkumbuke Yusufu na yule mnyweshaji wa kikombe cha Mfalme.

Hicho ndo kiwango na kipimo. Unachomkumbukia ndo alama kwako. Unamkumbuka kila unapokuwa na njaa au unapokula? Unamkumbuka kila unapotaka kusema uongo au unaposema kweli? Unamkumbuka kila unapotaka kumsingizia mtu au kumshuhudia kwa haki? Unamkumbuka ikiwaje.

By Raphael JL:
Dodoma.
0767033300.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.