Ads Top

AGANO LA KUMTAFUTA MUNGU KWA MOYO WOTE.


10.01.2018

Zaburi 119:10 “Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako?

Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Haya ndio maombi yangu leo. Nisaidie nisipotee. Kwa moyo, ndio sio kwa miguu. Kwa moyo, yaani kwa kule ambako chemichemi ya uzima inatokea. Kwa bidii yote, kwa shauku yote, kwa maarifa yote, kwa nguvu zote, kwa jitihada zote. Moyo hukaa mahali penye hazina. Kwa moyo wangu, ndio sio moyo wa mtu mwingine, sio kwa moyo wa rafiki yangu bali kwa moyo wangu. Kwa moyo wangu wote, sio nusu ya moyo au robo tatu ya moyo au asilimia 99 bali kwa moyo wangu wote. Kwa moyo wangu wote yaani kwa kila aina ya bidii na jitihada zangu zote, kwa ufahamu na akili zangu zote.

Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, yaani katika kumtafuta Mungu ni lazima kutumia moyo wote na sio vinginevyo. Yatupasa kumtafuta Mungu. Ahadi yake kwetu ni kuonekana kama tukimtafuta na sio kumtafuta tu bali kumtafuta kwa bidi. Hii bidii ya kumtafuta Mungu ndio ile kwa moyo wangu wote.  Kumtafuta Mungu ni kumtaka au kumuomba ajidhihirishe katika maisha yetu katika yale mambo tunayotaka msaada wake. Kwani kuna eneo tusilohitaji msaada wa Mungu? Hakuna. Basi yatupasa kumtafuta Mungu. Kumtafuta Mungu kunahitaji mapenzi ya kweli na ya dhati kwani gharama ni kubwa.

Ukisoma 2Nyakati 15:15, unaona inasema hivi, na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye Bwana akawastaheresha pande zote. Kumbe ndivyo inavyokuwa kuwa ukimtafuta Bwana kwa mapenzi yako au kwa kupenda au kwa shauku yako na ukampata basi yeye anakustaheresha, anakupa pumziko, anakupa burudiko, anakupa amani na utulivu pande zote au maeneo yote. Unapata utoshelevu wa kudumu maana umempata Mungu. Ni vema tukiangalie hiki kiapo kilikuwa kiapo cha namna gani. Tuendelee kidogo.

Ukiangalia msitari wa 12 wa kitabu hicho hicho cha 2Nyakati wa pili, utakuta maneno yanasema hivi; Wakafanya agano; ya kuwa WATAMTAFUTA BWANA, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote, na msitari wa 13 unaendelea kusema; na yoyote asiyemtafuta Bwana, Mungu wa Israel atauwawa. Hiki ni kiapo kigumu sana. Kwamba kila mtu ndani ya familia atamtafuta Bwana, kwamba kila mtu ndani ya timu au ndani ya nyumba au ndani ya kundi lazima amtafute Bwana. Hii inaonyesha kuwa kumbe kumtafutabwana ni lazima na ni jambo la kiungu kabisa. Mungu ameweka viwango vigumu sana vya kumtafuta na wote wanaolipa gharama ya viwango hivyo huwa wanapata thawabu.

Kumbuka kuwa kuna mambo hutayaona au kuna namna hutamjua Mungu kama hutalipa gharama ya kumtafuta kwa moyo wako wote. Ni maamuzi yako.



For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.