Ads Top

AIBU ZA KUJITAKIA HAZIHITAJI LAWAMA.



06.01.2018


Quotes by Raphael JL: Njia rahisi, njia ya ukweli, njia yenye ufanisi ya kukusaidia kukaa mbali na kupata aibu na kudharauliwa na kujidharilisha ni KUYAANGALIA MAAGIZO ya Mungu. Yaani kulishika neno, kuliishi neno na kulifanyia kazi kila siku. Hii ni siri ya ajabu. Kama unataka heshima, shika neno na lifanyie kazi. Neno la Mungu halisemi uongo. Mungu hadanganyi. INVEST IN THE WORD OF GOD AND BE EFFECTIVE.

Satisfied in Jesus, Fulfilled in Christ!

Zaburi 119:6 “Ndipo mimi sitaabika, nikiyaangalia maagizo yako yote”

Kuabika sio jambo zuri hata kidogo na wala hakuna mtu anaeomba wala kupenda kuabika. Aibu ni jambo la kudhalilisha. Ni jambo la kukufanya uonekane huna maana wala thamani. Aibu ni mbaya. Mzaburi anasema, yeye hataaibika akiyaangalia maagizo yote ya Mungu, vipi mimi na wewe? Tutapata heshima bila kumuheshimu Mungu kwa neno lake lote? Tutaponea wapi? Lazima tutaabika tu kama hatutamuheshimu Mungu. Hatuwezi kubaki salama kama hatutakuwa sawa na Mungu. Nasi leo, tunapewa changamoto ile ile ya kusema maneno yale yale, ndipo mimi sitaabika hakika kwani nimeyaangalia maagizo yako yote. Ni lazima yawe maagizo yote, sio nusu. Kama vile ambavyo hakuna uongo nusu au ukweli nusu. Ni lazima yawe yote. Inahitaji bidi. Kwa neema yake yeye atupaye bidi juu ya yote.
Ayubu 22:26 inasema, kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, na kuinua uso wako kumwelekea Mungu. Huu ujasiri hauwezekani kama mtu hayuko sawa na Mungu. Unaanzaje kuinua macho kwa Mungu na huku humuheshimu wala kukubali anachosema? Utajifurahishaje kwa Mungu usiyemuheshimu? Mungu ambaye kwa masaa yote 24 huna muda nae, huwezi hata kutoa basi fungu la kumi la masaa 24 ili uyatafakari mambo ya Mungu? Mungu ambaye kulisoma na kutafkari neno lake unaona uvivu ila kuangalia mpira na tamthilia kwa TV unakaa macho mpaka saa nane usiku? Tutapataje kupona pasipo kumjali Mungu anaetujali?

1Yohana 2:28, inakazia kusema, na sasa watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa mwe na ujasiri, wala msiabike mbele zake katika kuja kwake. Hili ni neno kubwa sana na zito. Mpendwa wangu, popote unaposoma maneno haya namuomba Roho Mtakatifu akupele kwenye kilindi na kina cha kuona upendo wa Mungu ulio wa ajabu sana kwetu kila siku. Tunahimizwa kukaa ndani yake au kwa lugha ingine kuishi ndani yake, huu ndo wito tulioitiwa. Ndani yake tuna amani na ujasiri. Matendo ya Mitume 17 inasema, ndani yake tunaishi, tunaenenda na tunao uzima. Kuishi ndani yake maana yake kuenenda katika njia za neno lake kwetu kila siku. Ni kukubali kufundishwa nay eye, kuelekezwa na Roho wake, kuonywa, kurekebishwa na kushauriwa.

Ndani yake tu sisi tuko salama. Nje yake ni aibu. Ila ipo aibu ile ya siku ile kuu ijayo karibu sana. Ile siku ya kuja kwake. Ili kuepuka aibu hiyo ambayo itakuwa ya milele basi imetupasa kukaa ndani yake. Hakuna namna ingine. Kiwango chako cha kukaa ndani yake ndio kinasema uwezo wako wa kutokuabika maana neno la Mungu linasitiri. Kuwa na neno la Mungu ni kama kujifunika blanket zito. Lakini liko neno la kuliangalia kidogo kwa kina. Lile neno, NIKIYAANGALIA MAAGIZO YAKO YOTE.

Lazima yawe maagizo yake yote. Lazima yawe maagizo. Maagizo haya ni mipango yote ya Mungu, ni taratibu zote za Mungu, ni mapenzi yote ya Mungu zinazoonyesha mamlaka na nguvu zake Mungu wetu Mkuu kwa watu wake na juu ya mambo yote anayotegemea kuwa sisi tutayafanya. Maagizo yake ni jumla ya neno lake lote na kila kinachopatikana ndani yake. Ipo gharama na Mungu atusaidie sana.

Kuyaangalia haya maagizo ni zaidi ya kukodoa macho kwenye biblia. Kuyaangalia ni kuamua kuyajua na kuyafuatilia ili uyashike na uyaishi kwa kuyatekeleza kila siku. Kuyafanya maagizo haya ni lazima uamue kabisa kwa kukusudia. Sio jambo litakalotokea kwa bahati nasibu. Ni lazima ukubali. Ni lazima uelewe. Ni lazima ufanye maamuzi ukijua ipo gharama. Kuyaangalia ni kuyatekeleza bila kujihurumia. Kijuhurumia ni adui mkubwa sana wa kuishi na Mungu na mambo yake. Usikwepe. Usikimbie kulipa gharama. Usiogope. Mungu hawezi kukuabisha kwa kuyaangalia maagizo yake. Atakusimamisha na kukufanya imara. Zingatia moyoni mwako. Aibu itakupata tu kama hutamuheshimu Mungu.

Ndio maana tunaona leo watu wanavyoabika kwa kuvaa vibaya wakisingizia utandawazi au fasheni. Ni aibu kudhani kuwa mavazi sio wokovu, basi ni heri kutembea uchi. Aibu kwenye maneno, maigizo ya kimaisha na kuiga maisha ya watu wengine. Ni aibu sana ikigundulika kuwa ulifaulu kwa kuigilizia mtihani. Ni aibu sana kwamba uliazima nguo na kwenda kujisifia kuwa ni yako. Kwanini upate mateso yote haya? SHIKA NENO LA MUNGU. MKATE WA UZIMA NAWE UTAKUWA SALAMA.



For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.