Ads Top

HUKUMU ZA HAKI YA MUNGU NDIZO HUZAA UNYOOFU WA MOYO KWA MTU.



09.01.2018

Zaburi 119:9
“Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako."

Kikawaida huwezi kusafisha njia safi. Ni lazima iwe imechafuka. Kwa hiyo kabla ya kuwa na haraka ya kuanza kusafisha ni lazima ujue huo uchafu umetoka wapi au nini kimechafua hiyo njia. Kujua nini kimechafua njia ya kijana kunasaidia sana kujua unasafisha kwa kutumia nini. Maana kuna uchafu hauwezi kusafishwa na maji tu au kufuta tu. Ndio hilo swali, "jinsi gani kijana aisafishe njia yake?"
Hii inamaanisha ipo njia sahihi ya kusafisha. Au zipo njia mbali mbali lakini ipo njia sahihi zaidi kuliko zote. Kumbuka kuwa kama mtu ni mchafu kwa nje anasafisha nje, vipi kama uchafu uko ndani ya mawazo na fikra zake? Huwezi kuyasafisha mawazo machafu kwa kuogelea kwenye maji au kujiacha ulowane kwenye mvua.
Lakini pia, ni muhimu kujua 'njia' ni nini ili itusaidie kujua namna inavyoweza kuchafuka na mwisho tukajua tunaisafishaje.

Mpaka kijana anaambiwa maneno hayo, ni wazi kwamba hili kundi la vijana ni muhimu na lina thamani ya pekee mbele za macho ya Mungu.
■ Kijana bado ana nguvu za kutosha akilini na mwilini. Akijihusisha katika kufanya jambo lolote anaweza kufanya kwa bidii na hamasa kubwa pia.
Akiwa mzuri anafanya mazuri kwa bidii na usahihi na kinyume chake pia.
■ Je, anaaminika kwa kiwango gani? Unaweza kumtegemea kwa kiwango gani? Hii ndo changamoto iliyopo. Lakini inaweza kufanyiwa kazi kwa kijana yoyote aliyekusudia kujifunza.

Kwahiyo, ni vema tukajua njia za vijana ni zipi na ni nini ili iwe rahisi kujua mengineyo.
'Njia' ni nini?
-Njia ya kijana ni yote anayowaza, anayopanga kufanya na anayofanya,
-fikra na maamuzi yake,
-namna anavyochagua kufanya au kutokufanya,
-maneno na matendo yake ya kila siku.
Haya ndiyo yanayo tafsiri utu, tabia na mwenendo wake.

Ukiitizama njia ya kijana kwa namna hii unaweza kuona ni njia zipi anaweza kuchafuka. Ukitazama kwa ndani utaona na kugundua kuwa milango sita ya fahamu inahusika sana hapo.
■ Mambo yanaingia na kutoka ndani ya kijana ndiyo yanayoathiri sana njia na mwenendo wake.
■ Mambo anayoona kwa macho yake ni taarifa zote zinazoingia ndani yake na zinaathiri sana namna atakavyofikiri baada ya kuona. Hii inamaanisha akiona uchafu basi macho yatachafuka na pia moyo utachafuka kwani macho yamepeleka taarfa chafu ndani.

Hivyo hivyo kwa masikio, mambo ambayo kijana anasikia yanaenda kutengeneza aina ya mtu.

Milango yote ya fahamu inahitaji ulinzi sana. Lile himizo la linda moyo wako kuliko yote uyalindayo linamaanisha pia kuwa lazima ujue moyo ni nini.
■ Na kumbe njia rahisi ya kulinda moyo ni kulinda mawazo na njia rahisi ya kulinda mawazo ni kulinda milango ya fahamu inayopitisha taarifa ambazo huwa mawazo hapo baadae.

Sasa hapo inaeleweka vizuri.
Kwamba, jinsi gani kijana asafishe mawazo yake, asafishe maamuzi yake, asafishe mwenendo na tabia yake?
Sasa ukijua mawazo huwa yanachafukaje ni rahisi kutafuta dawa ya kusafishia.
Hii inakuwa wazi sana sasa.

Turudi kwenye msitari wetu, Mkate wetu wa siku ya leo. Unasema, 'jinsi gani kijana aisafishe njia yake?' Ni kama kusema ameshagundua kuwa amejichafua, amejiharibu. Afanyaje ili arudi kwenye kusudi, arudi kwenye njia na arudi kwenye uhalisia badala ya kuishi kama nakala ya kuiga. Njia ya kurudi ni moja. Namna ya kusafisha ni moja. Jinsi ya kufanya ili aisafishe tena njia yake ni moja. Nafurahi kwamba kumbe kusafisha inawezekana., asante Yesu. Inawezekana kusafisha na kurekebisha njia zilizopinda na kuharibika. Yupo anaeweza kusafisha. Yesu. Kwani Yesu ndio neno lenyewe la Mungu.

Jinsi gani aisafishe njia yake? Mambo makubwa mawili yamewekwa hapo; kwa KUTII, akilifuata neno la Mungu. Maana yake anatii akiwa anaendelea kulifuata neno la Mungu linavyosema kwenye njia zake zote. Anatii na kuendelea kulifuata neno la Mungu. Analifuata neno, neno halimfuati kijana kwenye njia zake. Hii inamaanisha ni lazima kijana husika aamue mwenyewe kwa neema ya Mungu kulifuata neno. Hapo ndo utii unapimwa. Ukimpenda Mungu unalishika na kulifuata neno lake. Unampenda ndo maana unatii neno lake. Unatii neno lake ili uthibitike katika kumpenda yeye. Haya ni maamuzi ya kijana mwenye akili timamu. Kijana mwenye akili za smartphone au zile akili za popcorn hawezi kuona hili kuwa kubwa. Ataona anapoteza muda, ataona yeye sio mchungaji na kwahiyo hatakiwi kuwekeza kwenye neno la Mungu. Na ndio maana uko jinsi ulivyo.


UTII. UTII. UTII.

For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Maoni 1 :

Inaendeshwa na Blogger.