Ads Top

KIWANGO CHA UTII, KIPIMO CHA UTHABITI WA MWENENDO NA TABIA.



05.01.2018

KIWANGO CHA UTII, KIPIMO CHA UTHABITI WA MWENENDO NA TABIA

Quotes by Raphael JL: Kama ni gharama kutii basi ni gharama kupenda. Kama ni gharama kupenda basi ni gharama kuchagua. Ndio maana njia zetu, ili ziwe thabiti, yaani zithibitishwe na Mungu ni lazima kumtii Mungu, kulitii neno na Roho wake. Huwezi kutii kwa bahati mbaya au nzuri, ni lazima uamue kutii na hapo ipo gharama. Piga mahesabu ungetii, ungekuwa wapi leo?

Satisfied in Jesus, Fulfilled in Christ!


Zaburi 119:5 “Ningependa NJIA zangu ziwe THABITI, nizitii AMRI zako”

Yeremia 31:33, inasema hivi, bali agano hili ndilo nitakalofanya  na nyumba ya Israel, baada ya siku zile, asema BWANA; nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika;  nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Hiki ndio kipimo cha uthabiti. Hiki ndio kipimo cha kutokuyumba au kuyumbishwa.



Haya ni maombi mazuri sana. Ningependa njia zangu ziwe thabiti kwa kuzitii amri zako. Ni kama kuambiwa, njia zako zitakuwa thabiti kwa kutii amri za Mungu. Ni kama kumwambia mtu ambaye njia zake haziko thabiti kwamba akitaka kuwa thabiti ni lazima azitii amri za Mungu. Huwezi kuzitii kama huzijui. Kutii ni uchaguzi. Na leo, tunayo hiyo fursa ya kuchagua. Huu ni mwaliko mkubwa sana. Tumealikwa kuzitii amri za Mungu ili tuthibitishwe katika njia zetu.

Njia zetu ni nyingi na pana. Njia zetu ni mawazo na fikra zetu. Njia zetu ni maamuzi yetu ya kila siku. Njia zetu ni mikakati yetu. Njia zetu ni namna  yote kwa ujumla ya kuenenda kwetu kila siku mbele za Mungu. Njia zetu ni kila aina ya kukubali na au kukataa mambo mbali mbali au watu wanaoingia na kutoka maishani mwetu. Hizi njia au haya mambo yote yanatakiwa yawe imara na yathibitishwe. Na ili kuyathibitisha ni lazima kuzitii amri za Mungu. Kwa lugha ingine ni kwa kuzitii amri za Mungu ndio tunathibitishwa katika njia zetu. Matokeo ya kuthibitishwa na Mungu kwa kuzitii amri zake ni mengi na makubwa ikiwa ni pamoja na kupata kibali, kutegemeka na kuaminiwa maana njia zetu ziko salama kwa Mungu.

Kuwa thabiti ni kufanywa imara na mwenye nguvu za kutosha kushindana na kila ushindani unaokuja mbele yako kila siku. Kuwa thabiti ni kuwa na msimamo wenye nidhamu  unaokufanya kuwa mtu anaeaminika hata kimaamuzi. Njia zilizofanywa thabiti ni njia imara zinaoweza kukufikisha kwenye hatma ya unakotakiwa na unakostahili kwenda. Kuwa thabiti au kufanywa thabiti ni kuimarishwa, kutokutikisika, kutokuyumbishwa, kutokuwa na shaka wala wasiwasi yaani ni kuongezewa uhakika. Uthabiti ni nguzo ya Imani. IMANI THABITI. Kuwa na Imani thabiti ni lazima uzidi sana kutii amri za Mungu.

 Warumi 7:22,23, inahimiza sana kufurahia sheria ya Bwana kwa utu wetu wa ndani, yaani mtu akitupima kwa utu wetu wa ndani akute hiyo furaha, huo utulivu na utii kwa sheria za Bwana. Sheria za Mungu sio mzigo. Bila msaada wa Roho Mtakatifu utaziona ni mzigo kila siku. Kwa msaada wa Mungu inawezekana. Ingawa kwa sheria ya nje yaani katika mwili tunaona vita kubwa sana ya kumtii Mungu kwa neno lake. Ni kama kusema, ni rahisi kuwatii wengine kwa maneno yao na sio Mungu na ndio maana tunapata hasara za kutosha kila siku. Kama hujachoka kupata hasara kwa kutokumtii Mungu huwezi kuona umuhimu wa kumtii Mungu. Piga mahesabu ungekuwa thabiti kwa kiwango gani kama ungemtii Mungu kwa mwaka mzima? Ungefeli? Mahusiano yako yangeharibika? Ungekuwa unakopa pesa bila kulipa? Ungekuwa wapi?

Ni maombi yangu kuwa Mungu atatufanya thabiti kwa kutupa neema ya kumtii. Kulitii neno lake. Kumtii Roho wake. Unaweza hata ukaangalia tu kwa leo, ungetii ingekuwaje kwenye jambo lile na lile? Ungetii hakika ungethibitishwa. Kuthibitishwa kwenye njia zako maana yake ungefanywa imara zaidi na unakuwa ushuhuda wa namna Mungu anavyotembea na kuishi maishani mwako. Hakika ni furaha sana kuzipenda sheria za Bwana.

Kutii ni gharama kwani kutii kuko moyoni. Kutii ni gharama kwani kutii ni kupenda.


For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.