Ads Top

KUMTAFUTA BWANA KWA BIDII NI ISHARA YA UTII



02.01.2018

Zaburi 119:2 “Heri wazitiio shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wote”

Hii ni heri au baraka nyingine kwenye Zaburi ya 119. Baraka ni neno pana, pia humaanisha mtu anaemtafuta Bwana anapata amani na utulivu ambao dunia haiwezi kuuelewa. Amani na furaha ya kweli ambayo haiondolewi na vitu vya nje. Watu wanaofanya bidi katika kumtafuta Bwana wanazijua shuhuda zake, wanayajua matendo yake makuu na pia wanazitii. Kuna mambo kadhaa ya kutazama hapo. Huwezi kuzitii shuhuda usizozijua na kwahiyo ni vema na muhimu kujua kuwa upo umuhimu na gharama ya kulipa kuzjua shuhuda za Bwana. Baada ya kuzijua yatupasa kuzitii, yaani kuziishi na kuzikubali kwa kila kitu kinachosemwa nazo. Na haya yanawezekana kwa kumtafuta Bwana kwa moyo wote. Hapo kwa moyo wote inachukua kila kitu, haiachi kitu chochote, inachukua kila kitu ambacho kinatafsiri moyo. Yaani ni kumtafuta Bwana kwa nguvu zako, bidi yako, ufahamu wako, akili zako na vyote kwa ujumla.


Zaburi 112:1 utaona kuwa wale watu wamchao Bwana ndio wanaopendezwa sana na maagizo ya Bwana na hii inamaanisha kuwa kumtafuta Bwana kuna matunda mazuri na sahihi.  Hili ni agizo kubwa. Kushika shuhuda za Bwana. Ukisoma Zaburi 99:7, inasema wana wa Israel walishika shuhuda za Bwana. Ni wazi pia kuwa hata mimi na wewe leo tunatakiwa kuzishika shuhuda zake na kumtafuta Bwana kwa moyo wote. Hii ni kwasababu 1Nyakati 16:11, inaonyesha wazi kabisa kuwa kuna mambo makubwa mawili; KUMTAKA BWANA NA NGUVU ZAKE. Yaani katika kumtafuta Bwana, unatakiwa umtafute Bwana pamoja na nguvu. Kumbuka nguvu ni kwa ajili ya kufanyia kazi na sio kukaa tu. Kwahiyo unapotafuta sana kumjua Mungu ujue ni nini hasa unataka au unapotafuta.


 Zaburi 40:16, inasema hivi washangilie, wakufurahie, wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako waseme daima, atukuzwe Bwana. Kumbe kama sioni kufurahia na kushangilia katika kumtafuta Bwana inamaanisha kuna shangamoto. Ninapoweka muda wa kujifunza neno la Mungu, ninapotenga muda wa maombi, ninatakiwa niwe nafanya hayo yote kwa furaha na shangwe kwani ndio sehemu yangu. Tena Isaya anasem, tafuteni Bwana maadam anapatikana. Kumbe anapatikana. Hajajificha. Wale wanaomtafuta kwa bidii wanamuona na kutoa na kusimulia shuhuda zake.


Kumb 10:12 inatia sana moyo, ni swali la kujiuliza sana. Kwani Mungu anataka nini kwangu? Anataka nini kwako? Mungu hataki makuu au makubwa toka kwangu, amesema anataka mimi na wewe tumche na kumwogopa yeye, anataka tuenende katika njia zake zote, anataka tumpende, anataka tumtumikie kwa moyo wote na kwa roho yote. Tusiache kitu. Tusimtumikie tu kwa midomo. Mungu ni mwaminifu. Atusaidie na kutusimamisha tunapoendelea kutafakari Zaburi 119.


BARAKA NA UZIMA VIWE SEHEMU YAKO.

Wako katika Bwana,
Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.