Ads Top

KWENDA KATIKA NJIA ZA MUNGU NI TIBA THABITI YA UBATILI



03.01.2018

Zaburi 119:3 “Naam, hawakutenda ubatili, wamekwenda katika njia zake”

Wana heri wale ambao neno hilo la leo au Mkate wa Uzima huu wa Zaburi 119:3 linawaelekea wao. Wana heri wale ambao hawatendi kwa ubatili kwa kuwa wanakwenda katika njia za Bwana Mungu. Watu wanaoishi kwa kufuata njia za Bwana, kwa kufuata Neno lake ni watu wenye heri, ni watu wanaoishi kwa amani na utulivu na furaha. Ni watu waliotosheka sana. Wamebarikiwa. Ni maombi yangu kuwa, tunapotafakari neno hili la leo juu ya kutokutenda kwa ubatili na kwenda katika njia zake maisha yetu binafsi yatatiwa nuru ya kuona ni wapi tunatakiwa kubadilika na kumfanania Kristo mwenyewe. Pia tunaona kuwa bado ujumbe ule ule mkuu unaendelea tokea tulipoanza msitari wa kwanza wa zaburi hii ya 119. Kuna NJIA ZA BWANA, kuenenda kwazo kuna uzima na furaha. Huwezi kuenenda katika njia usizozijua. Kujua pia haitoshi, yatupasa kuzifanyia kazi hakika.

Ni wazi kuwa wale wanaolifuata NENO LA MUNGU, wanaoiishi na kulifanyia kazi kila siku wanaishi maisha mzuri sana. Watu hawa ni watu wa pekee sana maana kwao pia husemwa ile Zaburi 119:165 isemayo wana amani nyingi waipendao sheria yako, wala hawana la kuwakwaza. Hii inainua sana moyo. Neno la Mungu halisemi uongo na ni kweli kuwa mtu anaeipenda sheria au neno la Mungu anayo amani nyingi sana wala hana linalomkwaza. Hakika neno la Mungu ndio chimbuko halisi la maisha yenye utoshelevu kwa kila mwanadamu hapa duniani.

Mithali 3:1-2 inazidi kuonyesha umuhimu na thamani ya kuzishika  sheria na amri au neno la Mungu. Inasema hivi, mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. Maana ZITAKUONGEZEA wingi wa siku na miaka ya uzima na amani. Neno la Mungu halisemi uongo. Mungu si mwanadamu hata aseme uongo. Ni kweli kuzishika amri na sheria za Mungu kunaongeza siku za kuishi na kuleta amani. Hii ndio dawa na tiba ya kudumu ya msongo wa mawazo. Neno la Mungu linaweza kukupa tiba ya msongo wa mawazo. Lipa tu gharama ya Yoshua 1:8, mchana na usiku. Kila siku.

Neno ubatili maana yake ni kutenda kwa kiburi na majivuno ya hali ya juu, ni kutenda kwa kujihesabia haki na kwenda kinyume na uhalisia. Nawaza, hawakutenda ubatili bali walienenda katika njia za Bwana. Mimi na wewe pia, hatutakiwi kutenda ubatili bali tuenende katika njia za Bwana. Hii inamaanisha kuwa, kiwango chetu cha kuenenda katik njia za Bwana ndio kipimo cha utendaji wetu. Kuenenda katika njia za Bwana ni lazima tuzijue njia zenyewe ambazo zimefunuliwa kwetu ndani ya biblia na Roho Mtakatifu. Nani asiyejua analotakiwa kulitenda? Maana hata ndani ya moyo, upo ushuhuda wa sheria za Mungu.

Kila siku tunatakiwa kuenenda katika NJIA ZA BWANA. Zaburi 25:10 inakazia sana kusema, njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, kwao walishikao agano lake na shuhuda zake. Hii inamaana kwamba kama njia zangu hazionyeshi fadhili na kweli ni wazi kwamba sizishiki shuhuda za Bwana na kwahiyo lazima nitatenda ubatili. Kumbuka kuwa, haya yote yanafanyika moyoni, yaani ndani ya ufahamu wako. Yaani ndani ya mawazo na fikra zako. Mithali 10:29 inazidi kutupa ufahamu kwa kusema, njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu bali ni uharibifu kwao watendao maovu. Mimi na wewe, usalama wetu uko katika njia za Bwana. Njia za Bwana zimenyooka. Hazijapinda kama wasio haki wanavyosema. Hakika zimenyooka na zinajulikana kwao walio wanyoofu.

Hosea 14:9 una maneno haya makuu, ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana NJIA ZA BWANA zimenyoka, nao wenye HAKI watakwenda katika njia hizo; bali waasi wataanguka ndani yake. Mungu atusaidie sana. Usisahau kuwa Bwana Yesu ndiye NJIA PEKEE. Mpendwa wangu popote ulipo, zijue sana NJIA ZA BWANA ili uwe salama. Ili uishi kwa amani na utulivu.

Njia za Bwana zimefichwa ndani ya neno lake. Neno lake ndio mawazo yake. Ukitaka kujua mawazo ya Mungu nenda kwenye neno lake na kwa msaada wa ROHO MTAKATIFU utapata unono wa utajiri wake. Njia za Bwana ni mapenzi yake. Njia za Bwana ni mipango yake ambayo yote imefungwa ndani ya neno lake. Wekeza kwenye neno lake ili usije ukatwaliwa mateka na elimu za uongo za manabii wa leo.


BARAKA NA UZIMA VIWE SEHEMU YAKO.

Wako katika Bwana,
Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Maoni 1 :

Inaendeshwa na Blogger.