MAANDALIO YA MOYO NI YAKO, USIJIJIBU UKADHANI UMEJIBIWA.
26.01.2018
Zaburi 119:26 Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.
Ni kama vile Mithali 16:1 inavyosema, maandalio ya moyo ni ya mwanadamu bali jawabu la ulimi linatoka kwa Bwana. Hilo neno nitazisimulia linamaanisha kumwambia Mungu au kumpa mipango yako au kumwelezea njia zako au mipango yako na pia inaonyesha kuwa Mungu atajibu na katika kujibu huko kuna ombi la kuendelea kufundishwa amri zake. Bado tunaona msisitizo wa kutaka kufundishwa amri za Mungu kwenye maisha ya Mzaburi. Hii ni kiu ya ajabu sana.
Anaonekana pia kuwa alikuwa hana kitu cha kuficha mbele za Mungu na alijua pia kuwa Mungu atamjibu maombi yake na atamfundisha amri zake. Ninaamini kuwa Mungu anapenda na anafurahia sana akituona tunaonyesha nia na shauku ya kutaka kumjua zaidi hata kumuomba atufundishe njia za amri zake. Hiki ni kina cha ndani sana cha kumjua Mungu.
Mimi na wewe leo tujiulize kama tunayo shauku hii na kiu ya kutamani kuendelea kufundishwa neno la Mungu kila siku. Au shauku yetu iko wapi au iko kwa nani? Tunakumbushwa kumwambia Mungu mipngo na mawazo na njia zetu tukijua kabisa kuwa yeye Mungu atajibu maombi yetu. Hata leo tunaweza kumuomba atufundishe amri zake ili tusikosee katika maamuzi yetu ya kila siku.
For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.
Hakuna maoni: