Ads Top

MAISHA NI KUMTII MUNGU.



17.01.2018

Zaburi 119:17 “Umtendee mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.

Ni kweli kwamba kumtii Mungu ndio maisha halisi, yaani maisha nje ya kumtii Mungu hayana maana. Kumtii Mungu ndio maisha kwani Mungu ndio chanzo chake. Kila aina ya Baraka ambazo Mungu anaziachilia kwetu ni ili tuzidi kumtegemea na kumtii kwa kila hali na kila namna siku zote za maisha yetu. Hata watu wakiangalia maisha yetu waseme kweli sisi ni mfano ulio hai wa kizazi kinachomjua Mungu wao. Utii ni gharama. Tunaona maombi hayo kwenye Zaburi hii ya 119:17.

Mzaburi anaonyesha uhusiano uliopo ndani yake kati ya maisha na utii au kumtii Mungu. Anapomuomba Mungu amtendee kwa ukarimu ili apate kuishi ili aendelee kumtii Mungu ni wazi kabisa kuwa kumtii Mungu ndio maisha halisi. Kwa lugha nyingine ni sawa na kusema, mema na mazuri yote ambayo Mungu ananitendea kila siku kwa ukarimu wake ni ili niendelee kumtii yeye kwa kila kitu. Kama ninapumua leo basi ni ili niendelee kumtii Mungu kwa ile pumzi ambayo ndio uhai wangu. Maiti haiwezi kumtii Mungu maana haitambui lolote linaloendelea duniani au popote.

Utii ni kama mafuta yanayochochoea maisha yetu kuendelea kuwa na maana na thamani na tija mbele za Mungu. Tunatakiwa kutumia maisha yetu kumtii Mungu, kukubali anayotushauri maana hata hivyo yeye hatulazimishi bali ametuwekea utashi wa kuamua na kuchagua.  Utii ni kama chachandu au kitu kinachozidisha na kuongeza hamu ya maisha na huu utii ni kule kumtii Mungu tu. Utii ni bora kuliko sadaka. Kila unapotii kuna namna kumjua kwako Mungu kunaongezeka sana. Hii inakupa fursa zaidi ya kuendelea kufaidi mahusiano yako na Mungu. Vile ninavyowaza jinsi ambavyo mtoto mtii anafaidi vitu vya wazazi wake, vipi kwa Mungu Baba yetu? Japo kuwa ni gharama, ila utii ni jambo sahihi na zuri.

Gharama ya utii ndio inayotutenganisha hapa duniani kwani ingekuwa kumtii Mungu ni kama kusikiliza au kucheza mziki naamini kusingekuwa na utofauti kati ya wasanii wa nyimbo za injili na waabuduo halisi. Ni maombi yangu kwamba Mungu atupe utii.


For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.