Ads Top

MOYO USIO NA NENO LA MUNGU NI KICHAKA CHA UHARIBIFU.


11.01.2018
Zaburi 119:11 “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi?

Neno la Mungu linatakiwa kukaa moyoni, mahali ambako hazina ya maisha ya mtu inapatikana, mahali ambako chemchem ya uzima inatoka na mahali ambako nguvu za mtu ziko. Moyo ndio chimbuko la utu wa mtu na eneo linalotunza tabia na mwenendo wa mtu. Chochote kinachoanzia au kutokea moyoni ni halisi sana. Mithali 4:23 inasema linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, hii inaonyesha kuwa moyo ni muhimu kuliko vyote. Moyo usio na neno la Mungu hakika ni kichaka cha uharibifu kwani yanyotoka nje ni mambo yaliyojaa moyoni. Moyo ni muhimu sana. Ukiuchezea ni kama unachezea maisha yako yote. Moyo ni hatma ya mtu.

Hazina ya mtu ilipo ndipo na moyo wake utakapokuwepo. Kama hivo ndivyo basi ni wazi kuwa chochote unachoamua kitafsiri hazina kwako kitauvuta moyo pia uwepo mahali hapo. Hii maana yake, Daud alijua siri hii kuu sana. Aijua mahali sahihi ambapo Neno la Mungu linakaa, moyoni na akaomba na kuweka bidii katika kuliweka na kulitunza neno la Mungu moyoni mwake. Kumbe hii ndio dawa ya kushinda dhambi, kuliweka neno la Mungu ndani ya moyo wangu.

Moyo ukijaa unatoa kila kitu kilichokuwa ndani. Moyo wangu umejaa nini? Moyo wako umejaa nini? Ni rahisi sana kujua kuwa moyo umejaa nini kwani ukishajaa tu mawazo yanaanza kuathiriwa na kiwango kile kile cha uharibifu kilichoingina ndani. Moyo hauwezi unahitaji maarifa sana kuusimamia, ila kama Yeremia anavyosema kuwa ni Mungu tu anaweza kuushughulikia kwani moyo una ugonjwa wa kufisha na ni mdanganyifu. Moyo.

Neno la Mungu ndio njia pekee, ndio namna pekee ambayo tunaweza kuitumia na kuitegemea kama tunataka kuwa salama. Ukamilifu wetu ni neno la Mungu, nje ya hapo ni mateso. Jamani dhambi inatesa. Dhambi ni utumwa mbaya sana. Dhambi inaharibu kila kitu. Na dawa yake ni neno la Mungu. Neno la Mungu li hai na lina nguvu na ni kali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili. Waebrania 4:12 inasema wazi kuwa, neno la Mungu li jepesi sana kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Hii inatia moyo sana kwamba Mungu anajua kuwa moyo unahifadhiwa na neno lake pekee. Moyo wa mwanadamu hauwezi kuwa salama bila neno la Mungu. Mungu wa mtu hauwezi kuwa na amani bila neno la Mungu. Neno la Mungu ndio damu ya moyo.

Thamani huamua kiwango cha ulinzi pia. Ndio maana ili mtu asitende dhambi anatakiwa aliweke neno la Mungu ndani ya moyo wake kwani moyo wake una thamani na unatakiwa ulindwe na kitu chenye thamani kubwa kuliko chenyewe. Neno la Mungu lina thamani kuliko moyo, lina uwezo wa kuulinda. Moyo wangu hauwezi kulinda neno. Hii ndio siri. Neno lazima likae moyoni ili kunisaidia kushinda dhambi. Moyoni mwangu Bwana nimeliweka neno lako ili nisikosee. Hii ni kutokana na ukweli kwamba neno la Mungu linashauri na kuonya na kuelekeza.

EE BWANA NISAIDIE KULIPENDA NA KULITUNZA NENO LAKO MOYONI MWANGU ILI NISIKOSEE NA KUTENDA DHAMBI. AMEN.

For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.