Ads Top

NI WAJIBU WETU KUMTII MUNGU KWA BIDII YOTE



04.01.2018

Zaburi 119:4 “Wewe umetuamuru mausia yako, ili sisi tuyatii sana”

Hakuna wepesi katika kumtii Mungu, tena kwa bidii yote. Kumtii Mungu kwa bidii hufanywa kwa juhudi zetu zote, kulipa gharama zote na kufanya kwa hamasa kubwa sana. Hili jambo haliwezi kuwa jepesi au rahisi kwani ama sivyo lisingetakwa sana na BWANA kwamba tulifanye. Ni kama vile upendo wetu kwa Mungu unapimwa kwa utii wetu kwa neno lake. Maagizo yake kwetu ni kutii kwa bidii, kuyatii mausia yake, kulitii Neno Lake, neno linalotoka kwenye kinywa chake. Utaona hapo kuwa, sio kwamba anatuomba tutii bali anatutaka tutii maana huo ndio uzima wetu. Ni amri. Tumeamriwa kutii Neno lake maana pasipo kutii tutapata hasara za kutosha. Tunapaswa kutii sana, yaani kwa bidii na jitihada yote. Biblia imejaa mifano ya watu waliotii sana na kwa bidii na pia wale ambao hawakutii na wote wawili walipata thawabu yao. Namuomba Mungu atusaidie sisi tuweze kutii kwa bidii ili tufurahie mahusiano yetu na Mungu kila siku.

Kutii ni kuelewa. Kutii ni kukubali. Kutii ni kufanya. Kutii ni kupatia. Kutii ni kutekeleza maagizo kama ilivyoagizwa, pasipo kupunguza au kuongeza kitu. Kutii ni moja kati ya dawa za ubinafsi. Maana katika ubinafsi wangu ningetaka nifanye vile nionavyo kuwa ni sawa au hata kwa upendeleo ikibidi. Nimemkumbuka Sauli na Anania na Saphira. Ee Bwana nisaidie nisifanye EDITING KWENYE NENO LAKO ili nijisikie vizuri. Mungu ametuamuru au ametupa mausia yake ili tuyatii. Yaani tusipoyatii tunapoteza maana ya kwanini tumepewa hayo mausia. Kumbe yatupasa kuwa makini sana katika kutii mausia ambayo Mungu ametuamuru maana ni katika kutii ndio mapenzi yetu kwake yanakamilika. Kutii sio kuimba wimbo au kuandika kitabu au makala. Kutii ni kuyaishi yale ambayo tunaambiwa tuyatii. Bwana Yesu anasema mkinipenda mtazishika amri zangu (Yohana 14:15). Kumbe hata kupenda kumeshikwa na kutii. Kupenda ni kutii. Kutii kunaleta uzima. Kutii kunampa Mungu mamlaka juu yetu. Kumtii Mungu kunamfanya adhihirishe yale yaliyo ndani ya moyo wake kwa ajili yetu. Mtoto anayetii hupendwa na kupendelewa pia.

Yohana 14:23 inasema, Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, ATALISHIKA NENO LANGU, na Baba yangu atampenda, nae tutakuja kwake na kufanya makao kwake. Kumbe, Yesu na Baba yake hufanya makao ndani ya mtu mtiifu, anayetii neno lake. Anayeshika neno lake. Anayelitendea kazi neno. Kama kweli tunampenda Mungu tutashika neno lake, neno ndio kweli na kweli ndio Kristo mwenyewe. Kulishika neno la Mungu ni kuliishi na kulitendea kazi, kufanya yale neno linasema. Kama neno linasema SAMEHE basi samehe leo maana usiposamehe wewe sio mtii na huwezi kupata ile fursa ya Yesu na Baba yake kuja kukaa na wewe. Yesu na Baba yake hawawezi kuja kukaa mahali palipojaa kutokusamehe, mizaha na tabia za mwilini zote. Kumbe tunda la Roho ndio nyumba sahihi ya Yesu na Baba yake kuja kukaa.

Isaya 1:19 imeweka wazi kuwa, kama tukikubali na kutii tutakula mema ya nchi. Kama tukikubali kuwa sisi ni wakosefu na tukakubali ule wito mkuu wa toba na kugeuka, Mungu atatusamehe na kutuhesabia haki kwa Imani ndani ya damu ya Yesu. Tukikubali na kutii. Ni vigumu kutii bila kukubali. Unakubali kwanza na kisha unatii. Pia mkazo upo kwenye Kumbukumbu 28:1 unaosema hivi, itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, KWA BIDII, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, ATAKAPOKUTUKUZA juu ya mataifa yote ya duniani. Ukiendelea kusoma utaona kuwa kuna Baraka zinazoambatana na utii huu wa sauti ya BWANA. UKIONA UNABARIKIWA BILA UTII JUA HIZO BARAKA NI UHARIBIFU MKUU.

Ibrahim alimtii Mungu. Mpaka leo anaitwa baba wa Imani. Kumtii Mungu kunaacha alama ya vizazi vyote hakika. Yatupasa nasi kuomba neema hii ya utii. Mungu anajifunua kwetu kila siku. Ni wajibu wetu kutii sauti yake kama inavyofunuliwa kwetu siku kwa siku. Kumbuka kuwa ni ndani ya neno lake au sauti yake ndipo tunapata kila aina ya mwongozo na kuzijua amri na sheria na mapenzi yake kwetu. Huwezi kutii kama husikii vizuri. Huwezi kutii kama huelewi vizuri. Huwezi kutii kama huoni vizuri. Ni lazima milango yako yote sita ya fahamu ifanye kazi vizuri ndio utii unawezekana. Kumbuka pia kuwa kutii ni maamuzi binafsi. Kutii hakuji tu kama muujiza. Lazima uamue kutii. Ni muhimu kuamua kwani ipo gharama na kitu chenye gharama hakitokei tu kama mahindi ya kubabua.

Utii ni gharama. Angalia leo unayotakiwa kutii. Angalia neno la Bwana juu yako, juu ya familia yako na juu ya kila eneo. Huenda Bwana anakusemesha au alikusemesha kuhusu jambo fulani na mpaka leo hujafanya, hujaomba, hujamsaidia mtu au hujatimiza. Kutokutii ni hasara. Kumbuka, utii ni gharama. Ni heri kumtii Mungu kuliko kupata fedheha ya kutokutii. Namuomba Mungu atusaidie tuweze kutii.

UKIMTII MUNGU, UTAKULA MEMA YA NCHI.
Wako katika Bwana,
Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Maoni 1 :

  1. Tena ni hivi;Kutii ni silaha,Yakobo 4:7-8,Hatuwezi kumshinda shetani bila kumtii Mungu.Pia Kutii ni chanzo Cha baraka au laana.Kumtii Mungu ni chanzo Cha baraka,Kumb 28:1-.Ukumtii shetani ni chanzo Cha laana Mwanzo 3:1-

    JibuFuta

Inaendeshwa na Blogger.