Ads Top

SHERIA YA BWANA NDIO KAMILIFU NA UKAMILIFU



01.01.2018

Zaburi 119:1 “Heri walio kamili njia zao, waendao katika sheria ya BWANA”

Leo tunatafakari MKATE WA UZIMA wenye heri ndani ya sheria ya BWANA. Ni wazi hapo kwamba ipo heri au Baraka kwa kila mtu anaeenda katika sheria au NENO la Mungu. Hapo tuna kazi ya kujifunza na kutafuta, hata ikibidi kwa mifano, ni akina nani kwenye biblia walibarikiwa kwakuwa walienda katika sheria ya Bwana? Au walibarikiwa kwakuwa walishika NENO LA MUNGU? Je, na mimi leo nikienda katika sheria hizo nitabarikiwa na kupata kibali mbele za Bwana?

Mungu ameahidi kumimina Baraka zake na upendeleo wenye wajibu kwa wote ambao wamechagua kuishi kulingana na NENO lake na kulingana na viwango vyake vyote na miongozo yake. Mwanzo 26:3 kama alvyoahidi kuwa uwepo wake utakuwa pamoja nao, pia akitoa nguvu, msaada na ulinzi kama Waefeso 3:16. Kolosai 1:11 na Luka 24:50 zisemavyo. Unaweza pia kusoma Mwanzo 17:1,Kumbukumbu la Torati 18:13, Zaburi 128:1 na Zaburi 1:2. Kumbe kila mtu amchae Bwana na anaeenda katika njia zake amebarikiwa. Hii maana yake nini kwetu leo? Kumcha Bwana ni nini? Je, sheria ya Bwana inakupendeza? Maana huwezi kuenenda kwenye sheria inayokuchukiza na kukuboa? Unalifurahia NENO la Mungu na kulipenda? Unalitafakari NENO LA MUNGU usiku na mchana? Unaliruhusu NENO LA MUNGU liwe chimbuko la mawazo yako ya kila siku?

Hii inamaanisha ni lazima kujipima kila siku na kuona kama bado tunampenda Bwana kama mwanzoni au kama kuna namna yoyote ya uharibifu ndani ya mioyo yetu. Tukiwa wakamilifu katika njia za Mungu hakika tutmpendeza yeye nasi tutazidi sana katika kubarikiwa na kuongezwa na kufanywa imara. Yatupasa kukaa mbali na uhalifu wa kimawazo ambao ndio chimbuko la uharibu mpaka wa tabia na mwenendo.

Mithali 13:6 inakazia maneno yenye nguvu sana ambayo napenda tuyaone pia. Inasema hivi, haki humlinda yeye aliye mnyoofu katika njia zake, bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Haya ni maneno mazito sana. Kumbe ukiwa kamili katik njia zako sawa na NENO LA MUNGU linavyotaka na ukawa unaenda katika sheria za Bwana ni wazi kuwa unakuwa unaishi katika unyoofu ambao hata ikitokea shida basi ule unyoofu utaithibitisha haki yako. Vipi leo ukijichunguza njia zako unaona nini ndani ya ratiba na mambo yote umeshafanya mpaka sasa? Unamuona mwenye haki? Unamuona mtu mnyoofu ndani yako? Unamuona mtu anaependa sheria za Bwana na kuzishika?

Basi katika kuomba kwetu leo, tuombe Mungu atusaidie kuwa watu wanyoofu, atupe neema ya kutubu na kugeuka katika uhalifu wetu wa kila siku. Atusaidie tuende katika sheria zake kwa utii wa neno lake ili tuzidi sana katika kumpendeza yeye aliyetuita tuwe karibu nae. Kumbuka kuwa, kuwa mwenye haki na kuwa mtu mwadilifu kuna gharama yake, haitakuwa rahisi tu. Utalipa gharama. Utalipa gharama ya kuamua kumtii Mungu badala ya binadamu na hasa wakiwa rafiki zako wa karibu. Utalipa gharama ya kuzidi sana kuwekeza ndani ya NENO LA MUNGU ili uzidi kupata utajiri unaokufaa na kukusaidia kuzidi kumfurahia Mungu kila siku.

Sheria ya Mungu au NENO LAKE limeshathibitishwa kuwa linategemeka na linaaminika kwa vizazi vyote. Kiwango cha muda unachotoa katika kulitafakari na kuomba na kulisema ndicho kinachopima uwingi wa utajiri wa Mungu ndani yako. Lazima kulipa gharama ya kusoma NENO na sio tu kupitia kama unawahi kazini au unataka kulala. Kusudia kuanza safari hii na maamuzi magumu ila mazuri na sahihi ya kwenda na Bwana kwa NENO lake ili upate utoshelevu ambao dunia haina. SALAMU KWA FAMILIA YAKO NA HERI YA MWAKA MPYA WA 2018. FULFILLED IN CHRIST!


Wako katika Bwana,
Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.