Ads Top

NAKUPENDA KWA KIWANGO CHA KUJIFURAHISHA KWAKO



16.02.2018
Zaburi 119:47 Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, ambayo nimeyapenda.
Kujifurahisha inamaanisha kuwa na furaha kuu juu ya kitu, ni kufurahia uwepo wa kitu au mtu kwa kiwango ambacho hicho unachokifurahia kinakufanya uzidi kujifurahisha ndani yake kila siku unapokiona, unapokisikia au unapokigusa. Ni kiwango cha juu kabisa cha kumkubali na kumuelewa na kumpenda mtu au kitu. Ndipo unaweza kujifurahisha ndani ya huyo mtu. Kumbe tunatakiwa kufika hapo.

Hapo ni sawa na kusema hatuwezi kujifurahisha ndani ya maagizo ya Mungu, yaani jumla ya mambo yote anayotuagiza kama hatuyajui hayo maagizo yenyewe na kama hatumjui huyo Mungu mwenyewe anaetuagiza. Katika hili tunajua kuwa kupenda kwetu kumefungwa katika kutii neno au maagizo ya Mungu. Kama kweli tunampenda basi tutamtii na katika kuendelea kufanya hivi kila siku, ule upendo wetu unazidi kukua na ile furaha yetu inazidi kuongezeka pia sana.

Maagizo ya Mungu ambayo yako ndani ya neno lake yanafurahisha au yanazaa furaha ndani yetu kama tukiwa na mahusiano mazuri na mwenye maagizo kupitia Kristo na Roho wake. Haya ni maamuzi binafsi. Maamuzi ya kuamua kujifurahisha sana kwa maagizo ya Mungu. Hapo sasa utaona, bila kumpenda Mungu kwa kumtii hatuwezi kufurahia maagizo yake, yaani tutayaona ni mzigo mkubwa na hatutatamani hata kuyasikia wala kuyasoma wala kuyaona. Jiulize tu vizuri.

Jiulize tu vizuri juu ya vita iliyopo katika kusoma neno la Mungu na kulitafakari, unadhani tunampenda Mungu kwa kiwango cha kufurahia na kujifurahisha kwa maagizo yake? Hapa ndio njia panda ya mpitaji na msafiri. Tuna shauku na mambo mengine, tuna hamu na mambo mengine lakini sio neno la Mungu. Hapo hakuna utii wala upendo maana utii wetu kwa neno lke ndio kipimo cha upendo.

Kujifurahisha kwa maagizo ya Mungu hakutokei tu kama muujiza. Ni lazima ambo ya msingi yawe yametangulia ikiwemo kulipa gharama kadhaa ili tufike hapo na kubwa zaidi ni kulipa gharama ya kumjua Mungu. Kuijua Kweli. Hapo tukijua kuwa baada ya kujijua basi tutaifuata na kuitii n hiyo itazidi kukuza upendo wetu kwa Mungu.

For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.