WARAKA MAALUM KWA KILA KIJANA DUNIANI.
29.03.2018
Sehemu ya 01.
Jesus Up!
Kuna mambo yanawaangamiza vijana wengi duniani leo na ni vema yakawekwa wazi ili kuwasaidia wajue wanakoelekea na wanachotakiwa kufanya. Hii ni kwa vijana wote duniani, sio watanzania peke yake. Maana majira ya ujana ni kwa vijana wote wa kila namna bila kujali walipo na kama tukijali walipo basi utofauti hautakuwa ujana bali mazingira yanayowazunguka. Kuna mambo ambayo vijana wote duniani wanayatafuta kwa bidii nguvu zao zote hata ikiwezekana kutumia njia zisizofaa kupata hivyo vitu.
Sio tu vijana ila waraka huu ni kwa maalum kwa ajili ya vijana. Sio kwamba watu wazima hawasumbuliwi na vitu hivyo ila kwa sasa kundi linaloathirika zaidi ni vijana katika haya yote. Mambo kadhaa nimeyaona ambayo kama kijana asipokaa vizuri anaweza akajikuta anatumikia watu wenye mambo hayo na kujimaliza kwa sababu hiyo pia.
*Nini vijana wanahitaji sana?* Pesa, umaarufu, kuwa na watu wanaokusifia na kujiachia katika uhuru usio na mipaka. Humo ndani yake ni pamoja na kuvaa vizuri na kuonekana kijana wa tofauti anayemiliki simu za kisasa au kwa ujumla kuwa mtoto wa mjini. Waraka huu ni wa vijana wote, walio na wasio na dini kwani wote wawili ni wahanga wa jambo hili.
Vijana wengi wanapenda kuiga sana na hasa mambo wanayoyaona wao yanawavutia na kuyapenda. Wapo tayari kuiga hata mambo yanayowaumiza katika mchakato wa wao kuyafanya. Kuiga, ambako kimsingi kunaua ubunifu, imekuwa na changamoto kubwa sana kwa vijana ambapo kwa kupitia kuiga wengi sana wameharibika na kuharibiwa sana. Mathalani, ukiangalia nafasi na kazi ya mitandao ya kijamii na jinsi mitandao hiyo imetumika katika kuwasaidia na wengine kuwaharibu vijana ni wazi kuwa *uwezo mdogo wa kuchuja taarifa zinazotoka huko* imekuwa ni shida namba moja kwa vijana.
Angalau kijana wa kawaida ataiga kila kitu anachoona mtu maarufu amevaa au anafanya au anavyoongea bila kijana kujua kuwa maisha ya watu wengi maarufu sio halisi kwani kuna maisha yanayoonekana kwenye TV na yale yasiyoonekana kabisa au maisha nyuma ya pazia. Kuanzia kwenye muziki, mavazi, maisha kwa ujumla, vijana wamekuwa wahanga wa kuiga vitu vinavyowamaliza wao wenyewe. Kwa kutaka umaarufu na pesa, vijana wamejikuta wakiishi maisha ya watu maarufu ambayo kimsingi sio maisha yao na kubaki na maumivu makubwa kwenye maisha yao.
Ni rahisi kwa kijana kumuona mtu kama Kanye West au Jay Z au Beyonce au Rihhana au DMX na kuiga wanavyovaa kama ilivyokuwa kwa TUPAC wakati wake wa kuwepo duniani na namna alivyoathiri vijana wengi. Walikuwepo akina Michael Jackson na waliathiri dunia kwa asilimia kubwa sana lakini utajiri na mali na umaarufu wao haujawa na maana ukiacha maana ya kufahamika kama ni maana kweli. Yuko wapi Kanye West leo? Yuko wapi DMX leo au Ja Rule? Hii ni mifano michache tu ya namna uharibfu unavyofanya kazi.
Huwezi kuelewa mambo haya mpaka usikilize mashairi ya nyimbo zao ambazo zinaonyesha ni watu wanaolalamika sana kwa maisha wanayoishi na wengi hata kufika mahali kuimba kuwa wamezitoa nafsi zao kwa shetani ili wapate umaarufu na pesa na nyimbo zao zikubalike duniani. Ni vigumu kukubali lakini uhalisia unaonyesha hivyo. Vijana waliopo makanisani pia wameathiriwa na maisha ya namna hii mpaka na wao wameanza kutunga nyimbo zinazouza sokoni ili tu na wao wapate wanachokitaka. Ni mchanganyiko wa ajabu lakini unaeleweka mtu akiamua kuelewa. Watu wanaoonekana ni maarufu duniani ni watu wanaishi maisha ya upweke sana na hasa kwenye VIWANDA VYA SINEMA NA MUZIKI au maarufu kama MUSIC AND MOVIE INDUSTRY.
Ninachoelezea ni namna vijana leo wanahangaika kupata mafanikio ambayo yana vigezo na masharti yake sirini ingawa wao wenyewe hawaoni kama ni hatari kihivyo. Najaribu kusema kuwa wengi wa watu maarufu ambao ndio kama ICON za vijana kuwaiga wamefanya kila aina ya uharibifu ili kufika hapo walipo. Wengi sana wameua, wamelawiti na kubaka kama sehemu ya nadhiri zao ili waweze kupata pesa na kumiliki majumba ya kifahari. Huenda haya ninayosema hayapo Tanzania ila kwa uchunguzi wangu, nchi kama Marekani na hasa eneo la Hollywood maisha ya wasanii ni maisha ya masharti kama tu wanataka nyimbo zao zipigwe kwenye vyombo vya habari kwani wanaowamiliki wasanii ndio wanaomiliki vyombo vya habari pia.
Itaendelea….
Raphael JL:
www.ykm.or.tz
0787110003
Hakuna maoni: