KOSA LA WANA WA ISRAEL BAADA YA KUTOKA MISRI
Yuda 1.
Walipotoka tu Misri, wakavushwa na Mungu kwa mkono wake hodari na wenye nguvu katika bahari ya shamu walimsifu na kumwimbia sana Mungu na kumchezea. Maana waliuona wokovu wa Mungu aliye hai ulivyowatokezea mbele ya maadui zao na mbele ya bahari ya shamu. Hakika ulikuwa ni wakati wa kufurahi kwani Bwana ametenda muujiza wake. Hii inapatikana kwenye Kutoka 15.
Mbele tu kwenye sura hiyo hiyo wakafika mahali panaitwa MARA ambapo kulikuwa na maji machungu na wakashindwa kuyanywa maji hayo kwa ule uchungu wake na hapo hapo wakasahau kuwa Mungu waliyenae ni mkubwa kuliko MARA na wakaanza KULALAMIKA NA KUNUNG’UNIKA, wakamnung’unikia sana Musa wakisema TUNYWE NINI?. Na Musa akamlilia Bwana na Bwana akawapa maji matamu nao wakanywa na kufurahi tena kwa mara nyingine.
Sura ya 16, wameshasahu tena yale maji matamu na sasa wanakuja na ajenda ya maisha waliyokuwa wanaishi wakiwa watumwa kule Misri. Wakamnung’unikia Musa tena wakimwambia LAITI TUNGALIKUFA KWA MKONO WA BWANA KATIKA NCHI YA MISRI, hapo tulipoketi karibu na zile SUFURIA ZA NYAMA, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa?
Bado BWANA kwa uaminifu wake na wema wake AKAWANYESHEA MVUA YA MIKATE maarufu kama MANA kutoka mbinguni kila siku. Na ndivyo ikawa hivyo. Na yote haya BWANA aliyafanya ili watu hawa watambue nafasi ya Mungu kwenye maisha yao na kumfuata Mungu na sheria zake lakini kila walipopata changamoto kadhaa walimsahau Mungu na kuanza KULALAMIKA NA KUNUNG’UNIKA tu.
Sura ya 17, wakakutana na changamoto ya kiu maana hawakuwa na maji ya kunywa kwenye eneo walilofika lililoitwa REFIDIMU. Watu hawa wakateta na Musa na kumwambia TUPE MAJI TUNYWE. Hili kosa la sasa ndilo lililomfanya Musa kukosea na yeye na kukosa kuingia KANAANI maana naye hakufuata maelekezo ya Mungu kuhusu hili la maji. Mungu akawapa maji toka mwambani na wakanywa na kufurahi tena na kuendelea na safari. Lakini kwa upande mwingine jambo hili lilimfanya Musa aishie tu kusindikiza wengine.
Angalau kwa hayo machache unaliona kosa la wana wa Israel, KULALAMIKA NA KUNUNG’UNIKA na hasa kila walipokuwa wanakutana na changamoto fulani. Wanamsahau Mungu na kwenda kinyume na uaminifu wake. Kosa hili liliwafanya wana wa Israel wote kasoro watu watatu kutokuingia KANAANI maana walijaa malalamiko kwa kila kitu kilichokuwa kinaenda kinyume na walivyokuwa wanataa kiende.
Walikosa shukrani. Je mimi na wewe leo? Huu ni mwezi wa nne, leo ni siku ya kwanza ya mwezi huu, umeingiaje? Unakumbuka aliyokufanyia Mungu mwezi uliopita na kumshukuru? Au unasubiria ukutane na changamoto za mwezi wa nne uanze kulalamika na kunung’unika? Umemshukuru Mungu kwa mavazi yako au unaona ni kawaida tu kuvaa nguo na kupendeza? Umemshukuru Mungu kwamba umetoka kwenda kanisani au kutembea na kurudi bila kupata changamoto yoyote? Umeendesha gari bila ajali wala shida kwa mwezi mzima wa tatu, umemshukuru Mungu kukulinda na kukusaidia kufanya hayo au wewe ni mjanja sana maana una uzoefu wa udereva kwa miaka mingi?
Unakula chakula na kushiba hata kushukuru? Au ni kawaida tu? ANYWAY.
Kumbukumbu 8:11-20 inaweka wazi suluhisho la kosa hili:
Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka. Kama vile mataifa yale ambayo Bwana anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya Bwana, Mungu wenu.
EE BWANA NIONDOLEE MALALAMIKO NA MANUNG’UNIKO MOYONI MWANGU UKANITAKASE MOYO WANGU NA KUNIFANYA UPYA.
By Raphael Joachim Lyela
Web: www.ykm.or.tz
0767033300 (Whatasapp TU)
Dodoma,Tanzania.
Hakuna maoni: