Ads Top

NIPE MIMI HAO WATU NA MALI UCHUKUE WEWE.


26.04.2018
NIPE MIMI HAO WATU NA MALI UCHUKUE WEWE
Jesus Up!

Mwaka 2018 una kila fursa na sababu ya wewe kufanikiwa ikiwa tu utaishi na kuzingatia kanuni, hata hivyo *huwezi kuifaidi kanuni usioijua.* Kwa hiyo ni muhimu sana kama unataka kupiga hatua na kufanya vizuri basi ujue na uziishi kanuni. Moja kati ya kanuni ambazo lazima uzitekeleze mwaka huu ili usirudie makosa ya mwaka 2017 ni *watu*, ndio *kanuni ya watu*. Kama utakuwa umesoma masomo yangu mengine yaliyopita basi lazima utakuwa unaendelea kujenga stamina ya kukusaidia kuvuka mwaka huu kwa ushindi mkubwa. Kuanzia tarehe moja ya mwaka huu nimekuwa naandika somo moja la kukusaidia kwenda vizuri kwa mwaka huu na leo nakuongezea jambo hili kuu kuhusu watu. Kama nilivyosema watu ni kanuni, utawategemea tu hata kama una pesa , kimsingi huenda ni watu hao hao ndo walikufanya uwe na pesa. Nilishasema kuwa *hata uwe na maono makubwa kuliko mlima Kilimanjaro kama hujui namna ya kuishi na watu basi hutaenda popote pale.*

Mwanzo 15, ina stori ya babu Ibrahim ambayo nataka niitumie kusemea jambo la leo. Ibrahim aliungana na baadhi ya wafalme kwenda kupigana vita na upande wake ukashinda na kuteka nyara mali nyingi tu. Wakiwa wanarudi njia Mfalme wa Sodoma akamwambia Ibrahim “NIPE MIMI HAO WATU NA HIZO MALI UCHUKUE WEWE” na Ibrahim alimkatalia hilo ombi lake. Nataka nitumie hayo maneno ambayo ndiyo kichwa cha somo ili nizungumzie umuhimu wa watu maishani mwako kwa mwaka 2018. Huyu Mfalme wa Sodoma lazima kuna kitu cha tofauti alikiona kwa hao watu mpaka akawa tayari kuacha mali zote ili awapate wale watu waliokuwa na Ibrahim. Kikawaida, watu wangetaka mali na sio watu maana *mali zina udanganyifu wake na usipokuwa makini zinaweza kukutoa nje kabisa.* ```Kwanini aliwataka watu na sio mali?```

Baada ya Mungu, ni watu. Watu ambao hata Mungu mwenyewe hafanyi kitu bila wao, kimsingi sio kwamba hana uwezo wa kufanya bila wao ila ni kanuni hiyo. Watu toka unazaliwa mpaka unakufa. Watu ndio waliokuzaa, wazazi, na watu watakuzika. Watu ndio waliokuinua na kukuangusha kwa nyakati tofauti au zinazofanana. Watu walilia pamoja na wewe na wakakucheka badae. Watu wanakusifia sana na kukulima kuwa huna lolote na hasa ukiwa haupo walipo. Watu wanaomba msaada wako na wewe unaomba msaada wao. Watu ndo unawahitaji mwaka huu baada ya MUNGU KWANZA. Watu ndo utafanya nao kazi maana katikati yao wamo wateja wa bidhaa na huduma zako lakini pia wamo maadui wa biashara yako. Watu wakikuamini watakutumikia hata kama ni mambo ya kijinga ili mradi umefanikiwa kuwashawishi wakakuelewa. Watu ndo watatumiwa na adui kukuharibia, kukukatisha tamaa, kukuvunja moyo na hao hao wanatumiwa na Mungu kukuinua na kukutia moyo.
Jiulize, nini unacho ambacho watu hawajahusika? Kuzaliwa kwako wapo watu walihusika, kukua kwako wapo watu wamehusika, kusoma kwako wapo watu wamehusika, kufanikiwa kwako wapo watu wamehusika. Kama una watu wa namna hii maishani mwako *USIWABADILISHE NA MALI AU MAFANIKIO.* Wapo wanaotumia watu kwa nguvu za giza, wanawatoa kafara ili wapate mali, hawa ni vipofu na wapumbavu katika ubora wao. Hawajui kuwa mali si kitu mbele za watu. Hawajifunzi wenzao walivyofanya, walikataa mali ili wapate watu, watu wenye faida na thamani. Hii ni siri nzito. Mwaka 2018 una watu wengi sana wanaoweza kukusaidia kukamilisha hatma ya maisha yao, Mungu anawajua wote na kwahiyo ukianza na MUNGU KWANZA ni wazi kuwa Mungu atawaleta wote unaostahili kukutana nao kwa mwaka 2018 na mwisho wa mwaka utakuwa na sababu milioni moja za kumshukuru Mungu kwa kukuletea watu uliotembea nao kwa mwaka mzima.
Hata kama huna maono bado unahitaji watu, ukiwa na maono ndo kabisa, unahitaji watu wa kukusikiliza, watu wa kukuelewesha, watu wa kukutia moyo unapokata tamaa, watu wa kukushauri unapokuwa njia panda, watu wa kukuonya na kukumea unapopotoka, watu wa kukutegemea kama unavyowategemea. Kimsingi unahitaji watu. Unapopita katika vita na magumu unahitaji watu wa kupita nao ama sivyo unaweza kujikuta umeishia njiani na ukakosa mwelekeo. Wakati mwingine unahitaji tu mtu wa kusema pole, au wa kukwambia hongera umefanya vizuri ili uweze kuendelea kupiga hatua nyingi mbele yako. Si kweli kwamba unahitaji pesa, kumbuka pesa na fursa zote wanazo watu yaani watu wamewekwa kama kanuni usiyoweza kuiepuka kwa njia yoyote. Vitu vyote unavyotumia ni kazi za watu, sasa nini unadhani si cha watu?
Ukitaka kufanya sherehe unahitaji watu, kukiwa na msiba lazima watu wahitajike, ukihitaji bidhaa lazima utaipata kwa watu na huna namna nyingine. *Ndio maana kuwajua watu na kuishi nao kwa uangalifu ni jambo la msingi sana.* wewe kama kijana, pamoja na kwamba unausaka umaarufu kwa gharama ya ujinga wako mwenyewe ngoja nikwambie hakuna mahali unaenda kama hujui kuishi na watu. Utahitaji watu wanunue kazi zako. Uzuri ni kwamba Mungu aliyewaweka watu yupo na yeye ana mamlaka juu yao, kwahiyo badala ya kupambana tu peke yako mshirikishe Mungu anaeweza kugeuza mioyo ya watu ikusaidie usije ukajichosha bure.
Watu hawafanani, hakuna anaebisha. Hawafanani kwa kila kitu, maumbile, uwezo wao wa ndani na hata namna wanavyofanya mambo yao hata kama wana elimu na umri sawa. Mwaka 2018 kusudia usije ukawadharau watu wasioonekana nadhifu kama wewe maana kumbuka wao ni fursa unayohitaji kwa mwaka huu. Wapo watu waliowadharau wengine kwa maumbile yao na kesho wakagundua kuwa wanawahitaji sana. huna sababu ya kumdharau mtu kwani wewe huna uwezo wa kumuumba au hata kumbadilisha yaani awe mrefu kama wewe. Fahamu tu kuwa kila mtu ambaye Mungu anamruhusu kuja kuwa karibu na wewe ni lazima unamuhitaji, wengi kwa kutokuja wamewafukuza watu wa namna hii mbali nao na maisha yao yakaendelea kuwa yale yale ya *historia za kufanikiwa* mwaka uliopita na *majuto ya kushindwa mwaka huu.*
Bwana Yesu alipokuja duniani alihitaji watu, na katika wengi akawachagua 12 ambao akawa anakuwa nao na kuwafundisha na hawa 12 ndio wale waliobeba maono ya Yesu Kristo hata baada ya yeye kuondoka. Bwana Yesu alijua thamani ya watu ingawaje yeye ni Mungu lakini bado hakuwa tayari kupata mali na badala yake alitafuta watu. *Wewe ni nani usiyetaka watu?* Kumbuka kuwa kati ya wanafunzi 12 wa Yesu, ndani yake alikuwemo Yuda aliyemsaliti, alikuwepo Petro aliyemkana na wote walikuwa sehemu ya watu walikokuwa karibu sana na yeye. Huu ni ukweli usiopingika kuwa, kati ya watu unaotembea nao mwaka 2018 wapo wazuri na wabaya, na wote wana kazi na kusudi la kutimiza kwako. Unahitaji hekima ya kujua namna ya kuishi nao.
Mwaka 2018, Mungu akukutanishe na watu wote unaostahili kukutana nao, watu wote ambao ni sehemu ya kusudi la Mungu kwako, watu wote ambao ni sehemu ya hatma ya maisha yako. Mungu akupe macho ya kuwaona na kuwatambua na kutengeneza mahusiano nao katika namna itakayokufaa. Unaweza hata ukawaandika mahali, watu ambao kukutana nao kumebadilisha kabisa maisha yako na namna ambayo inaonekana ili inapofika mwisho wa mwaka unaweza kuwatambua pia. kumbuka Mungu hufanya kazi pamoja na watu na vitu vyote alivyotupa ni kwa ajili ya watu, wewe kama mtu fanyika msaada na Baraka kwa watu wengine wanaokuhitaji ili mwisho wa mwaka uwe na ujasiri wa kusema NIPE MIMI HAO WATU na mali uchukue wewe maana watu ni hazina yenye utajiri mkubwa ziadi kuliko mali.

YKM: Satisfied inJesus, Fulfilled in christ

Raphael JL
+255 787110003
Dodoma, Tanzania

Insta: @raphaellyela
Youtube: Raphael JL
Web: www.ykm.or.tz
Www.fichuka.blogspot.com

Maoni 1 :

Inaendeshwa na Blogger.