TOFAUTI KATI YA MSANII WA NYIMBO ZA INJILI (GOSPEL ARTIST) NA MWABUDU (WORSHIPER) part 2
05.04.2018
Na Pst. Raphael JL
[PART 2]
Tuendelee….
Kwanza, mwabudu halisi ndiye anaetafutwa na Bwana mwenyewe, Yohana 4:23-24 na wala hapo Bwana hajasema ANAMTAFUTA MWIMBAJI. Uwe unaimba au hauimbi unaweza ukawa Mwabudu Halisi. Kuchanganya au kulinganisha KUMWABUDU Mungu kwa kumaanisha ni kuimba, nalo ni jambo la ajabu sana.
Kuimba au muziki kuna nafasi yake lakini sio kila kitu ingawa ukiangalia kwa upana utaona ni kama kuimba na muziki ndivo vinavyotafsiri KUMWABUDU MUNGU. Kuna watu wako makanisani, hawajui kuimba wala kupiga vyombo lakini wanatumia KILA MWENYE PUMZI AMSIFU MUNGU MINISTRY na kwa kweli wanamwabudu Mungu wa kweli katika roho na kweli.
So ukiona unaupenda muziki na unapenda kuimba kuliko unavyopenda kuimarisha mahusiano yako na Mungu ujue kuna jambo gumu liko ndani yako. Ni sawa na kupenda MIKONO YA MUNGU KULIKO KUUPENDA MOYO WAKE. Mwabudu halisi anawekeza sana kwenye kujenga mahusiano yake na Mungu na anajua kuwa vyote alivyo navyo amepewa na Mungu.
Mwabudu halisi haimaanishi yeye hana KIPAJI ila kwake kipaumbele ni MUNGU KWANZA maana hata kipaji chenyewe alipewa na Mungu so KIPAJI hakumfanyi ajione kuwa yeye ni wa pekee dunia nzima like there is no one else like him or her. Yeye hakiabudu KIPAJI wala hauabudu MUZIKI wala haabudu KUIMBA bali anajua hivyo vyote ni muhimu sana katika mchakato mzima wa kufanya ibada na kumwabudu Mungu kila siku.
Mwabudu halisi anajua hata akiwa peke yake chooni au bafuni hajisahau yeye ni nani na ndo maana anakuwa makini KUJITUNZA ili asijikute ameingia kwenye changamoto za kujichua. Haimaanishi amekamilika ila ni mtu anaeishi akijua hana cha kuficha hata kama ametenda sirini. Ni mtu mwepesei kukubali kosa lake na kutubu na kugeuka na kuamua kuacha mambo yasiyofaa.
THE AUDIENCE OF A TRUE WORSHIPPER IS GOD AND HIS PRESENCE.
Waabudu halisi wanajua kuwa IT'S ALL ABOUT GOD, yaani haimaanishi hawawajali watu bali watu pia wanatakiwa kufundishwa ili wajue KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO NA KWELI ni nini badala ya kukaa na kusubiria. Ndo maana wengi hudiriki kusema kabisa kuwa YAANI SIJABARIKIWA KABISA NA HUYU KIONGOZI WA IBADA, huyu mtu anatakiwa afundishwe kujua ANAEABUDIWA NI MUNGU na ikifika hapo kila mtu anatakiwa amwabudu Mungu (Kumbuka sijasema anatakiwa AIMBE AU APIGE MUZIKI, huku najua nafasi ya muziki na uimbaji katika kumwabudu Mungu)
Mwabudu Halisi, kama ni kiongozi wa uimbaji na muziki kanisani anajua nafasi yake lakini moyo wake uko kwa Mungu kwani hiyo ibada sio ya kuwafurahisha watu bali ya kumgusa Mungu. So anapofanya huduma na kazi yake mbele za Mungu hataki kutumia UZOEFU WAKE WA KIPAJI NA MATAMASHA kumaliza kazi yake.
Mwabudu halisi hana muda na MASHINDANO kwa namna yoyote kwani yeye ATASHINDANA NA NANI WAKATI ANAFANYA KWA MUNGU? CAN HE OR SHE COMPETE WITH GOD? MASHINDANO YANATOKA WAPI? So mwabudu Halisi anajua hafanyi kwa mashindano, hajipimi na mwingine, wala haangalii kazi za dunia ili na yeye atengeneze kazi yake, wala havai ovyo ovyo tu kwa tiketi ya USANII au kuwa MAARUFU. Mwimbaji halisi anajua hana sababu ya kutafuta umaarufu kwani tayari yeye ni maarufu sana MAANA ANAJUA KWANZA ALITAFUTWA NA MUNGU NA PILI AMEPATIKANA NA MUNGU, HUU NI UMAARUFU UNAOTOSHA KULIKO WA KUGOMBANIA KUSHINDANIA TUZO.
Wengine husema kuwa mashindano kama hayo ni kwa ajili ya maendeleo ila ukiangalia kwa undani utashangaa sana vita na chuki na majivuno na maringo na kiburi na uchungu unaozaliwa kwa sababu ya hayo yote. Mwabudu halisi ANAJUA KUWA ANATOSHELEZWA NA MUNGU.
Ukweli ni huu, wapo watu wengi maarufu wenye kila kitu, wenye tuzo zote za Oscar na Grammy na zote zingine uzijuazo lakini bado hawana UTOSHELEVU. Wanahangaika mpaka sasa, na kwa kuwa ni watu maarufu wanaonekana kama wako vizuri maana hata wakituma picha zao kwa mitandao ya kijamii wanaonekana wanatabasamu. Lakini ndani yao wanaungua.
Mwabudu halisi hawaigi watu wa mataifa wanavyofanya, hawaigi akina Beyonce au Rihana. Fuatilia uone kinachotokea kwa watu hawa wanaoonekana kuwa ndio INTERNATIONAL ICONS, fuatilia ujue akina Tyrese wana hali gani leo ili ujue huenda watu wanaopenda kutafuta umaarufu kwa njia ya GOSPEL wakawa hawajui wanachotafuta ni nini.
Lazima ufahamu kuwa MIFUMO IMETENGENEZWA KUTII MAMLAKA ILIYOITENGENEZA. Waandaji tuzo wanajua kwanini, wana nia yao, sembeuse kushinda unadhani watu huwa wanashinda tu kiholela kama mfumo hauwataki? Kamuulize Kanye West. Anyway. Nisemacho ni kwamba kuna mifumo ya dunia imeingia kanisani na inaonekana kuwa ni sawa na ukisema sio sawa wewe unaepinga ndo unaoenekana sio wa kisasa. NI HERI NIBAKI MSHAMBA PAMOJA NA YESU.
Mwabudu halisi hasubiri matukio tu. Hasubirii matamasha tu. Maana yeye humwabudu Mungu kama sehemu ya maisha yake ya kila siku, akiwa anakula, akiwa anajisaidia chooni, akiwa kwenye gari, akiwa na furaha, akiwa na changamoto, akiwa amepata au amekosa bado ATAMWABUDU MUNGU kwani anajua WORSHIP IS A STATE OF AN ATTITUDE AND NOT SEQUENCE AND SERIES OF MUSIC AND SINGING.
Nalazimika kuishia hapa. Nimelazimika.
MUNGU AWE PAMOJA NASI ZOTE.
By Raphael JL
Web: www.ykm.or.tz
0787110003
Dodoma, Tanzania
Instagram: @raphaellyela
YouTube: Raphael JL_
Hakuna maoni: