VITA YA IMANI KATIKA KIZAZI CHA TAARIFA.
VITA YA IMANI KATIKA KIZAZI CHA TAARIFA
Huwezi kuelewa mpaka uelewe. Zamani watu wenye imani waliishindania imani kwa damu zao, yaani wengi waliuwawa, walipigwa na kuteswa sana ili kuthibitisha mapenzi yao kwa Mungu katika Yesu Bwana. Leo kuna baadhi ya maeneo vita ya mwilini bado ipo lakini si kama ilivyokuwa zamani.
Ulimwengu wa leo, vita yake ni mbaya zaidi kuliko hata ile ya mwilini kwani imeenda kwenye taarifa na wengi hawaoni kuwa ni kitu. Kama vita imehamia kwenye taarifa maana yake sayansi na teknolojia ina sehemu kubwa sana leo. Pia kama vita imeenda kwenye taarifa ina maana vyombo vyote vya taarifa vinahusika sana. Wewe angalia tu...!
Ni kweli humuoni adui akija kimwili lakini angalia matumizi ya simu, runinga, mitandao na vyombo vyote vya taarifa. Kuibuka kwa mitandao ya kijamii, michezo mbali mbali kwenye runinga kumeharibu si tu mtu mmoja mmoja bali na familia kwa ujumla. Baba anagombania rimoti, mama anataka rimoti, watoto pia. Kila mtu anataka cha kwakwe.
Mazungumzo ya familia yamevamiwa na chatting za kwenye mitandao ya kijamii mpaka kwenye vitanda. Watu wanalala na simu zao pembeni, sio biblia tena. Hali ni mbaya na ngumu. ADUI KABADILISHA NAMNA YA KUPAMBANA. Ndio maana Waefeso 6:11 inasema kuhusu HILA ZA SHETANI. Sasa kanisa linapoa au limepoa? Vita ya taarifa huwezi kuipigana kimwili. Ni lazima uipigane kiroho maana taarifa zote ni roho na zinaathari kubwa rohoni. Ndo maana wewe angalia tu...!
Angalia shauku na kiu na njaa ya kumtafuta Mungu, angalia maombi na kusoma Neno la Mungu. Angalia watu wako kwenye maombi huku wanachati kwenye simu zao. Watu wako kwenye ibada mpaka waambiwe wazime simu. Yaani utulivu haupo tena. Nguvu zimenyonywa sana. ADUI KAHAMISHA UWANJA NA NAMNA YA VITA YENYEWE. Umewaza taarifa za mashuleni na vitabu vinayvoandikwa? Familia zimevurugwa, ushoga, usagaji na mengine mengi sasahivi yanafundushwa kwa kutumia katuni, movies na michezo mbali mbali.
JE, BADO UNA IMANI ILE ILE? UNAZIDI KUKUA KATIKA IMANI YAKO?
Ukiwa unachati uko macho.
Ukiwa unaangalia mpira uko macho.
Ukiwa unapitia mitandao ya kijamii kwa simu yako ya kisasa uko macho.
Ukiwa unaangalia movie uko macho.
Ukiwa unaangalia michezo ya kihindi na kifilipino na mingineyo iliyotafsiriwa kwa Kiswahili uko macho.
KILA KITU UKO MCHO KASORO...!!?
Maombi yakianza unalala. Ibada ya nyumbani ikianza ghafla usingizi na uchovu unakuvaa. Muda wa kusoma na kutafakari Neno ukifika utulivu na hamu inaondoka. Ukifika tu muda wa mambo ya Mungu kila shauku na hamu na njaa inaondoka na badala yake unakuja uvivu, uchovu na usingizi na mtu akijifanya anaomba kwa muda mrefu unaweza hata kumchukia.
KANISA LA NYUMBANI LIKIPIGWA, KUSANYIKO LA KANISANI HALINA NGUVU.
BADILIKA. BADILISHWA. BADILISHA.
Raphael JL:
www.fuchuka.blogspot.com
Instagram: raphaellyela
Jesus Up.
Hakuna maoni: