MISULI YA UONGOZI LEADERSHIP MUSCLES.
MISULI YA UONGOZI.
LEADERSHIP MUSCLES
Misuli ya uongozi ni zile nguvu ambazo kiongozi anazipata baada ya kupita au kupitishwa kwenye changamoto kadhaa na akavuka salama. Ni ule ujasiri unaozaliwa ndani ya nafsi ya kiongozi ambao ni matokeo ya kuvuka kwa uaminifu katika mchakato fulani mgumu wenye uwezo wa kuzaa ujasiri. Ni ule ushupavu na umakini, ni ile nguvu ya ushawishi ambayo inazaliwa baada ya mchakato husika kukamilika. Ukimuona kiongozi unaemfurahia na kumpenda kwasababu ya uimara wake ujue ametengenezwa na mchakato na lazima alikubali kuivishwa mpaka mwisho.
Wengi hupenda nafasi ya uongozi kwa sababu za ubinafsi wao, wengi wana uchu wa madaraka na mali wanajua kwa kupata nafasi fulani ya uongozi basi watafaidika. Ni viongozi wachache sana wanaokuwa viongozi kwa nia ya dhati ya kufanya wajibu wao kwa watu. Duniani, kwa sasa tuna viongozi wawili, angalau kwa kiasi kinachoonekana ambao wanafanya kazi zinazoonekana kuwalenga wale wanaowaongoza, nao si wengine bali ni rais mwenye asili ya biashara wa Marekani Bw. Donald Trump na rais wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli. Hawa wote, pamoja na wengine ambao wameshikilia ajenda ya mataifa yao au kujenga mataifa yao kwanza, wanapita katika vipindi vigumu sana vya kusemwa vibaya na watu. Hapo wanajengwa ile misuli ya uongozi wao.
Majuzi nilimsikia rais Donald Trump wa Marekani akisema, ni sehemu ya majukumu yake ya kazi kusemwa vibaya na watu na hasa wale ambao wanajitanabaisha kwamba hawakumchagua na hasa upande wa chama pinzani cha Democrats. Kuwa na mtazamo kama huo kunampa ahueni kubwa sana ya kujenga misuli ya uongozi katika kuwaelewa na hata kuwashinda adui zake. Pamoja na yote hayo yanayotokea bado kile anachofanya ni kwa faida ya Wamarekani wote bila kujali dini zao, makabila yao au imani zao katika siasa. Kufanya hivi pasipo ubaguzi kwa watu ambao wanakupinga sio kitu rahisi sana ila ni lazima misuli ya uongozi ijengwe.
Wengi hudhani uongozi ni ile nafasi au cheo ambacho mtu anapata au anapewa au anatafuta na ndio maana wengi wao wamejikuta wanapata vyeo na nafasi hizo hata kwa kujidhalilisha na rushwa. Kila uongozi ulioko ndani ya mtu, yaani ile nguvu ya ya kushawishi lazima itapitishwa katika mchakato wa kuivisha na kuizaa na kuikomaza misuli yake ya uongozi. Kuongoza watu wanaokaribia milioni 60 kwa nchi kama Tanzania sio jambo jepesi ingawa kwa ushabiki mtu anaweza kudhani ni kama kuwa kiongozi wa darasa la watu 50. Ni lazima uwe na misuli ya kiuongozi na kama huna hiyo misuli basi lazima ukubali ijengwe na wakati wa kujengwa hiyo misuli unaweza usifurahie sana kwani huo mchakato wa kujenga una mambo magumu sana.
Kujenga misuli ya uongozi inatakiwa iwe moja kati ya tunu za kiongozi mahali popote pale. Mtu anapowaza kuwa kiongozi ni lazima ajue gharama yake kwanza ili anapokubali ajue amekubali nini. Hata ukiwa kaka au dada mkubwa kwenye familia na unachukuliwa kuwa wewe ni kiongozi ni lazima uje kuwa ipo gharama ya kulipa ili kudhihirisha uongozi wako. Mahali popote ulipo, iwe ni kwa nguvu ya ushawishi wako au nafasi au cheo kuna namna wewe ni kiongozi. Fikiria uongozi katika kiwango cha juu kabisa duniani, yaani kujiongoza mwenyewe. Kwenye kiwango hiki cha uongozi hutegemei kukuta mtu anakula ndizi halafu anatupa maganda barabarani, maana anajua fika kuwa sio kila barabara ni jalala au ni eneo la kutupia uchafu. Na ndio maana ukiwa unasafiri ukafika mji kama Moshi, mpaka akili inakwambia tu kuwa lazima uwe makini na unaona kabisa kuwa kuna namna ipo nidhamu iliyojengwa kwa sheria. Misuli ya uongozi.
Inawezekana upo kwenye idara ambayo watu hawakuelewi, iwe ni kwa kutaka kwao au kwa utendaji wako. Unaweza kufika mahali ukakata tamaa na kuona huna kitu cha kufanya au hata ukatamani kuhama na kwenda kwingine. Ambacho wengi hatujui au huwa tunasahau ni kwamba hata ukienda kwingine, watu huambiana mabaya na mazuri yetu na hasa mabaya kwa namna ambayo unakoenda unaweza ukakuta faili lako limeshafika. Kumbe dawa sio kuhama. Dawa ni kukaa kwenye mchakato wako ili misuli yako ya uongozi ijengwe hapo. Na moja ya msuli ambao kiongozi yoyote lazima awe nao ni msuli wa kutosumbuliwa na maneno ya watu. Kwamba watu wataongea hilo linajulikana. Ni wajibu wako wewe sasa kusimama juu ya maneno ya watu mpaka wale watu wanaokusema wafike mahali wajiulize kama wewe ni mtu wa kawaida mwenye masikio au la. Ni lazima uwe na msuli wa kutoyumbishwa na maneno ya watu.
Hili la maneno limewavunja viongozi wengi na hasa kama yanayosemwa ni kweli. Kama yanayosemwa ni kweli ni vema ukayafanyia kazi na kubadilika ili tabia yako na mwenendo viwe nguzo ya uongozi wako. Ukisingiziwa kitu kwenye uongozi wako ujue ni tabia na mwenendo wako ndio utakaokuja kuthibitisha kuwa wewe ni mwenye haki, ila ukiwa na tabia za ajabu na ukawa huna maadili basi hapo utakwama sana. Lazima ukubali hali halisi ya mambo yanayotokea katika eneo lako la uongozi. Kiongozi anaruhusiwa kusingiziwa na kusemewa maneno magumu. Ni kazi yake na ni wajibu wake. Na hayo maneno yote yanatakiwa yawe ya kusingiziwa kweli kweli ili kiongozi husika apate nguvu na ujasiri wa kusimama na kuendelea na kazi wakati maneno yanaendelea. Ni kweli kwamba kelele za chura haziwezi kumzuia ng’ombe kunywa maji lakini kama zitamzuia basi lazima ng’ombe awe amekubali sana.
Nawatia moyo viongozi wote ambao mnatimiza wajibu wenu katika mazingira magumu ya kusemwa vibaya na watu hao hao mnaowasaidia. Msiwalilipizie kisasi. Bwana Yesu alisema wapendeni adui zenu, hiyo inawamaliza nguvu adui. Bwana Yesu mwenyewe alikuja kuwasaidia watu hapa duniani lakini hao hao walimkataa na kumuua. Wewe usidhani uko peke yako. endelea kutimiza wajibu wako wa msingi. Usisahau kuwa hapa duniani ni rahisi sana kukumbukwa ukiwa haupo kwani ndio maana ya kukumbuka, sasa wewe ishi kwenye kiwango cha kuonekana wa maana na wa thamani ukiwa hai bado. Kumbuka kupingwa sio kuzuiwa. Ni raha zaidi kupingwa na watu walio karibu na wewe au wale wanaokufahamu zaidi kwani hata adui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.
KUBALI KUJENGA MISULI YAKO YA UONGOZI ILI UWE KIONGOZI MWENYE MOYO WA MUNGU.
NB: Tuma kwa kila kiongozi unaemfahamu duniani ili kuwatia moyo viongozi wetu.
Raphael JL
www.fichuka.blogspot.com
Jesus Up
Hakuna maoni: