THE YARDSTICK OF TRUTH :FUNGU LA KUMI.
Ibrahim ndiye mwanadamu wa kwanza kutoa FUNGU LA KUMI kwa Melkizedeki (Yesu kama unataka kuamini). Alitoa fungu la kumi kabla ya torati au sheria kuandikwa. Alitoa fungu la kumi kwa ile sheria ya neema ndani ya moyo wake. Alitoa fungu la kumi kwenye mamlaka kubwa kuliko yeye. Baadae watoto wake wa mwilini pia walitoa, kwa mfano Yakobo. Watoto wake wa imani je? Fungu la kumi linakupa shida? Ujue haipo neema bali sheria na sheria ina kazi yake pia. Kama wewe ni mwana wa Ibrahim kwa imani na baba yako alitoa fungu la kumi kabla ya sheria, kwanini sheria ikupe shida leo mpaka uone kutoa fungu la kumi ni biashara ya wachungaji as if walianzisha wao? Tumlaumu Ibrahim, wala sio Musa. Neema ipo, kwanini kukaa chini ya kongwa? Asili ya fungu la kumi ni utii kwa Mungu, kumtambua Mungu kuwa anamiliki vyote na amekupa vyote. Soma Mwanzo 14 yote.
Hata Ibrahim alitoa fungu la kumi kwa Kuhani na Mfalme Melkizedeki ambaye alikuwa mfalme wa Salem (Yerusalem ya kale sana). Wewe kinachosumbua ni nini? Unapotoa unaamini unampa mchungaji na sio Mungu wa Mchungaji? Huu ni utofauti mkubwa sana. Wajibu wa Melkizedeki ulikuwa kumbariki Ibrahim baada ya kutoa. Wajibu wa Ibrahim ni kile alichofanya baada ya kufunuliwa Melkizedeki ni nani. Wapo wanaofundisha kuwa fungu la kumi ni jambo la agano la kale, wamejuaje? Biblia ina maagano mawili tu na yote yanamuhusu mtu mmoja; YESU KRISTO. Manabii wote waliandika habari za Yesu. Hakuna aliyeandika habari za Yesu kipande au mguu peke yake. Agano la kale ni kuu kuu kweli lakini haimaanishi halina kazi au halina maana au halifai maana hata Yesu mwenyewe hakuna kuliondoa bali kulifanya lieleweke zaidi, kulifanya liwe na maana zaidi. Yaani kuna mambo tusingeyaelewa kuhusu agano la kale kama Yesu asingekuja.
Agano la kale ni zaidi ya torati au sheria alizopewa Musa. Agano la kale ni ujumla wa mahusiano yote ya Mungu na wanadamu kwa majira na nyakati zile. Ni jumla ya namna zote ambazo Mungu aliamua kujidhihirisha na kutembea na wanadamu wa wakati ule. Ila ufahamu kuwa kabla ya sheria za Musa kuandikwa alikuwepo Ibrahim, baba wa imani ambaye aliishi kwa neema ya wakati huo na kumtolea Mungu pasi na sheria bali vile ambavyo moyo wake ulifunuliwa kuona na kufanya. Ni lazima mtazamo ubadilike na ngome ivunjwe ndio utaweza kuelewa kuwa vita ya fungu la kumi imekaaje. Ukiendelea kuamini kuwa unatoa fungu la kumi na kumpa huyo mtumishi utaendelea kujisikia vibaya na kuumia sana maana huyo ni mwanadamu tu. Lakini ukifika kwenye uhalisia wa chimbuko la fungu la kumi toka kwa baba yetu wa imani Ibrahim, utafanya kwa bidii ya moyo wako.
Mwanzo 14:18-20
Baada ya kutoka vitani Ibrahim (Abram) anakutana na kuhani na mfalme wa Salem, Ibrahim anapewa mkate na divai, taswira ile ile ya mwili na damu ya Yesu na kisha Melkizedeki anambarikia Ibrahim akisema hivi “Abram na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abram AKAMPA FUNGU LA KUMI LA VITU VYOTE. Alijua ule ushindi alioupata ni Mungu kamsababishia na kumshindia. Wewe unadhani una nguvu kiasi gani cha kushinda yote ambayo unakutana nayo kila siku? Mpe Mungu heshima yake. Habili na Ibrahim watoshe kutufundisha kuwa utoaji wa sadaka na fungu la kumi ulianza hata kabla ya sheria na torati ambayo ndio inaleta vita kati ya kanisa. Hao wawili watoshe kuwa mfano tosha. Lakini bado unao uchaguzi wako na usisahu lile swali la Mungu kwa Kaini, KAMA UKITENDA VYEMA HUTAPATA KIBALI? Mwanzo 4:7. Sio kila kutenda tu bali kutenda vyema. Nani alimfundisha Habili kutenda vyema kwenye utoaji wa sadaka? Nani alimfundisha Ibrahim kutoa fungu la kumi kwa kuhani Melkizedeki ambaye Waebrania 7:1-10 inazisema habari zake kwa jambo hili tu?
IBRAHIM ALIISHI KABLA YA SHERIA. SISI TUNAISHI BAADA YA SHERIA. WOTE WAWILI HATUKO CHINI YA SHERIA.
Raphael JL
www.fichuka.blogspot.com
Jesus Up
Hakuna maoni: