UTAJUAJE KUNA UHARIBIFU UMESHAFANYIKA MAHALI.
Inaweza kuwa kwenye familia, urafiki, mahusiano, kazini, katika biashara au kwenye jambo lolote. Kuna hali ukiziona ujue lazima kuna uharibifu umeshatokea na huenda unaendelea kutokea. Wengine hudhani ni hali ya kawaida lakini nikwambie kuwa sio hali ya kawaida. Hali ya kawaida ni asili katika ukamilifu wake. Mfano kama Mungu hakuumba uharibifu ina maana lazima uharibifu ulisababishwa. Nina mifano michache kwenye maandiko inayoonyesha ishara kadhaa za kwamba uharibifu ulitokea au ulikuwepo. Ngoja tuziangalie kwa pamoja.
HALI YA UKIWA NA UTUPU: MATHAYO 12:25
Ukisoma huu msitari utaona muunganiko wa ishara mbili katika viwango tofauti. Moja ni ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake yenyewe utabakia UKIWA. Ukiwa sio hali nzuri hata kidogo. Lakini unaona hapo kuwa FITINA INAZAA UKIWA. Ufalme ni kama kusema nchi, nafsi ya nchi ikifitinika juu yake yenyewe basi hali itakayokuwepo ni ukiwa, ukiwa ni kiwango cha uharibifu. Ukiwa sio upweke. Ukiwa kwenye hali ya ukiwa maana yake uko kwenye hali ya kuachwa, kutokuzingatiwa, kudharauliwa nk. Hali hii ya ukiwa pia inaonekana katika Mwanzo 1:2.
Ukiwa ni hali mbaya sana, ni hali ya kupungukiwa na kuondokewa na Maisha, furaha, amani na hata uchangamfu wa moyo.
Kwa kuwa hali ya ukiwa pia inamaanisha kuachwa, basi utupu lazima utakuwepo tu, yaani mtu unajiona kabisa kutokutosheka. Japo kwamba unaonekana kuwa na vitu vingi lakini ndani yako upo utupu ambao unakufanya mpaka usione maana ya Maisha. Kuwa na mali nyingi hakuondoi utupu kwani hali hii ya utupu ni zaidi ya kile kinachoonekana kwa nje. Huu utupu ni hali ya uharibifu wa ndani ambao unakufanya ujione huna kitu hata kama una kila kitu. Utupu unatakiwa ujazwe ili ulete maana. Inajalisha sana ni nini unajaza ndani yake.
HALI YA KUTOSIMAMA
Hapo hapo utaona sehemu ya pili ya Mathayo 12:25 inasema, nyumba au mji ukifitinika juu ya nafi yake yenyewe HAUTASIMAMA. Kwa lugha ya kawaida kabisa kutokusimama maana yake hakuna kinachosonga mbele, hakuna kuendelea, hakuna uendelevu. Unafanya mambo mengi lakini huoni kuimarika, kila siku unaona bado kufikia lengo. Hakuna kinachosimama, unaanzisha vingi na vyote vinaishia njiani. Unaanzisha mahusiano lakini yanaishia njiani, unalipiwa kabisa mahari au unalipa kabisa mahari lakini hakuna ndoa. Unaanza kabisa biashara lakini haiendi popote. Unagusa hiki na kuacha kile ukiamini labda huko utafanikiwa, unaanza vizuri tu lakini katikati unakwama. Hapo mpendwa ujue upo uharibifu unatafuna.
HALI YA GIZA:
Mwanzo 1:2
Ipo hali ya giza na kwa tafsiri hii, fikiria mtu aliyeko gizani, ni kweli ana macho lakini hawezi kuona, ana miguu lakini atatembeaje gizani asikojua anakoelekea? Ulishamsikia mtu anasema YUKO GIZANI? Maana yake hajui nini cha kufanya, maana yake amechanganyikiwa, maana yake haelewi achukua hatua gani. Hali hii ya giza haijalishi mtu ni msomi, masikini au hali yoyote aliyonayo kwa sababu hii haionekani kwenye ulimwengu wa mwilini kirahisi.
TUNATOKAJE KWENYE UHARIBIFU
Jambo la muhimu kulifahamu kabla hatujajifunza namna ya kutoka kwenye uharibifu ni kwamba Shetani anaitwa baba wa uongo, mfitini na mtu wa hila nyingi sana. Ndie anaepanda mbegu ya uharibifu ndani ya Maisha ya watu mpaka kuwavuruga watu, maana yeye hapendi watu washikamane na ndio maana anavunja ndoa za watu kwa kushirikiana nao. Shetani, katika yote ayafanyayo ni kuhakikisha ANACHINJA, ANAHARIBU NA KUUA ikibidi. Haya matatu ndio kazi yake na ukiyaona popote ujue ni kazi yake. Ila Yesu Bwana wetu alikuja ili ATUPE UZIMA, TENA UZIMA TELE. Yesu ndiye suluhisho la kila uharibifu wa yule muovu kwenye Maisha yetu. Mkimbilie leo nawe utakuwa salama.
Katika kutoka kwenye uharibifu, utaona kwanza unahitaji NURU kama Mwanzo 1:3 inavyosema. Unamuhitaji Yesu maana yeye ndio hiyo Nuru. Unahitaji kufunguka ufahamu wako ili uyaone Maisha katika macho ya mbinguni na sio duniani tu. Hii Nuru itakufundisha na kukusaidia kuyapima Maisha yako na kuamua kutoka kwenye hivo vifungo kwa jina la Yesu. Muombe Mungu akurehemu na kukusamehe, fanya toba na ugeuke. Amua kusimama kwenye nafasi yako ili baada ya wewe asiwepo mwingine wa kupita kwenye njia ya uharibifu hata kama ramani ya uharibifu imeshachorwa.
UFUNIKWE NA AMANI YA KRISTO YESU IPITAYO FAHAMU ZOTE.
By Raphael JL: 0767033300
www.fichuka.blogspot.com
Jesus Up!
Asante kwa ujumbe mzuri, neema ya mungu itufunike, pia tumtafute mungu kwa bidii
JibuFuta