Ads Top

NGUVU YA KUTAFAKARI MAUSIA YA BWANA.


15.01.2018

Zaburi 119:15 “Nitayatafakari mausia yako, nami nitaziangalia njia zako?
Mungu alimwambia Yoshua, katika Yoshua 1:8, kuwa kitabu cha torati au biblia au neno la Mungu halikutakiwa kuondoka kinywani mwake, na ya kwamba alimtaka ayatafakari maneno yaliyomo ndani yake kila siku, mchana na usiku. Mungu anajua kabisa kuwa kufanikiwa na kusitawi kwa sisi kama watoto wake kumefungwa ndani ya neno lake njia ya kupata hekima na kanuni na maarifa ya kutufanikisha ni kwa kutafakari maneno yake yaliyomo kwenye biblia kwa msaada wa Roho wake. Hii inahitaji kulipa gharama.

Nguvu ya kutafakari neno la Mungu au kuyatafakari mausia yake yanayopatikana ndani ya neno lake inapatikana  kwa kutenga muda na kulitafakari neno. Kutafakari ni matokeo ya kuwekeza katika neno kwa kulisoma, kuliomba na kuliishi. Kutafakari ni zaidi ya kufumba macho na kukunja sura na kukaa kimya. Kutafakari ni kulipitisha neno katika fahamu zetu na mawazo yetu ili kwamba yale yanayotoka yafanane na neno lenyewe. Hapo lazima tufanikiwe na lazima tuwe na majibu.

Unapotafakari unamaanisha unatoa muda wa kuruhusu neno la Mungu lipite ndani yako, likulowanishe na kukutosheleza katika njia za moyo wako kwa kiwango ambacho unakuwa na uwezo wa kuepuka uharibu ulio nje yako. Kumbuka, ukiliweka neno la Mungu moyoni mwako litakusaidia kushinda mitego ya dhambi; na usisahau kuwa tamaa huzaa dhambi na dhambi huzaa mauti. Kiwango cha tafakari huwa kinadhiirishwa na nguvu ya unachotafakari kwenye maisha ya kawaida. Yaani unachokitafakari huwa kinapata nguvu zaidi kadri unavyotafakari.
Kutafakari sio jambo rahisi kwani linahitaji utulivu na muda. Pia lazima ndani uwe umekusudia maana haiwezi kutokea kwa bahati mbaya au nzuri. Ni lazima ukusudie. Na hapo kwenye kukusudia ndipo penye gharama. Kuna vitu utalazimika kuviacha ili tu upate muda na wakati mzuri wa kuwekeza ndani ya neno la Mungu. Kitu chochote unachokipa muda mrefu kukiwaza na kukichakata ndani ya fikra na mawazo yako ndicho kinachosema wewe utatoa mambo ya aina gani. Neno la Mungu linatuumbia utu na tabia ya Mungu ndani yetu. Mausia ya Mungu yanapatikana ndani ya neno lake.

Daud pia aliweka nia ya dhati katika kuziangalia njia za Mungu. Na hii inaonekana wazi kuwa kwakuwa ameahidi kuyatafakari mausia ya Bwana, kinachofuata hapo ni kuyazingatia, ni lazima kuweka msimamo juu yake. Name nitayatafakari mausia yako; hii inaonyesha wazi kabisa kuwa Daud alijua kuwa jambo hili ni la kila siku, ni la wakati ujao, ni la mpango yaani lazima kujipanga kuyatafakari mausia ya Bwana. Hii inazaa nia ya dhati ya ndani ya kuziangalia au kuzitilia maanani njia za Bwana. Hii iwe shauku na maombi yetu kila siku.


For the King and His Kingdom,
Pastor Raphael JL:
0787110003.
DODOMA.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.